Ijumaa. 26 Aprili. 2024

Tafakari

Jumapili, Septemba 18, 2022

Hekima katika kutumia ya Dunia

Mwenyezi Mungu huwainua wanyonge toka katika mavumbi yao. Tunapaswa kutambua kwamba sote ni watumishi wa jamii yetu na hivyo tusiache kuwaheshimu wote, hasa wanyonge ndani ya jamii yetu. Karani dhalimu anatambua kwamba atapaswa kuirudia jamii na hivyo anajifunza kurudisha urafiki na jamii yake. Zaburi ya wimbo wa katikati toka katika Zaburi ya 113 inatuambia: “Msifuni Bwana anayewakweza maskini.” Waliokwezwa na Bwana ni wana wa Israeli tangu walipochaguliwa kama taifa teule na baadaye kukombolewa utumwani Misri. Wanafunzi wa Bwana Yesu nao waliimba maneno ya Zaburi hii jioni ile kabla ya kuteswa kwa Yesu (Mk 14:26).

Katika somo la kwanza, Nabii Amosi anatoa onyo kwa matajiri wa Israeli waliowanyanyasa maskini. Ipo siku Mwenyezi Mungu atawainua maskini hawa. Utajiri haupaswi kututenga na jamii bali yafaa ujenge urafiki wetu na jamii. Bwana Yesu katika injili anatutaka tuanzishe urafiki, sio tu na jamii yetu bali zaidi na Mwenyezi Mungu kwani mambo ya dunia hayadumu.

Yesu anatoa mfano wa karani aliyeogopa fedheha ya umaskini. Alitumia cheo chake dakika ya mwisho kuanzisha urafiki na wachache. Yesu anamsifu huyu karani wa leo kwa sababu gani? Alikuwa mjanja, alijua kwamba hatma yake ni kurudi kwenye jamii na hivyo akajitengenezea watu wa kumkumbuka.

Yesu anasifu kwamba huyu karani alijua kutumia mali ya dunia vizuri. Lakini lengo la Yesu ni kutuambia kwamba makao yetu ni mbinguni. Tutumie muda wa duniani kuandaa ya mbinguni. Tumia mali, elimu, biashara na kipaji chako katika kuandaa makao haya. Tutambue kwamba kuna maisha baada ya cheo au mali.

Msaada wetu unapatikana kwenye jamii yetu pia. Hivyo, tusizisahau jamii zetu. Mungu huwashusha wenye kiburi na kuwapandisha wanyenyekevu. Tunaalikwa kuwa watu wa kubadilisha hali mbaya za maisha na kuzifanya kuwa njema.

Sala: Njoo moyoni mwangu, Ee Bwana na upafanye sehemu yako ya kuishi,

Amina.
----------------------
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni