Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Septemba 13, 2022

Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu leo. Leo basi neno la Mungu linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na tafakari kwamba karama zote zipo ndani ya Kanisa ili zilijenge Kanisa; Mungu huwaita watu mbalimbali-wengine huwafanya mitume, manabii na wengine waalimu. Anataka wote hawa wasaidie kila mmoja kwenye nafasi yake kuujenga mwili wa Kristo; yaani kanisa.

Lakini basi huko Korintho waliona ukuu hasa katika karama ya kunena kwa lugha mbalimbali. Wale waliofanikiwa kwa hili, walijiona kwamba ndio watakatifu wenyewe, ndio rafiki wa karibu zaidi na Mungu na hivyo wanauwezo wa kuamua chochote kuhusu wengine. Waliokosa uwezo huu-walidharaulika-hivyo kila mtu akaanza kutamani karama ya kunena kwa ndimi. Paulo anakaa chini, anaona kwamba hapa pana upotofu mkubwa-Paulo alitambua kwamba mwanadamu hupewa karama fulani na Mungu kwa sababu tu ya huruma au upendeleo wa Mungu-kweli unakuta huyu mwanadamu hastahili, ukiangalia matendo yake, maisha yake, busara zake, makandokando yake unakuta ni mengi lakini unashangaa kwamba Mungu kampa karama fulani au kipaji fulani.

Mfano: unaweza kukuta kwamba mtu fulani ni mlevi ajabu lakini uwezo alionao kiakili hapo kichwani ni mkubwa ajabu-au unakuta kwamba mtu anamajivuno ajabu au hata ni mlevi kupindukia lakini bado Mungu kamjalia uwezo wa ajabu na ujuzi wa udaktari wa kutibu wa ajabu au uhandisi wa ajabu. Yeye akishatokea tu-tatizo linatatuliwa. Hapa unaweza kujiuliza-je, huyu anastahili kupata yote haya?-kweli unatambua kwamba hastahili, ni Mungu tu kaamua kumpatia na kampatia kadiri Mungu mwenyewe alivyoamua.

Hata wenye hizi karama za uponyaji-unakuta baadhi wana karama lakini maisha bado yanaudhaifu. Ukitafakari yote haya utagundua kwamba ama kweli mwanadamu hana cha kujivunia. Anachopaswa tu ni kuonesha upendo-ili basi aweze kujenga mwili wa Kristo.-Kutumia ile karama kwa faida pia ya wengine kama wakili mwema wa karama za Bwana. Hivyo upendo unakuwa ndio fadhila kuu kuliko zote kwani Mungu anatoa ili aangalie kwamba je, tutashirikishana katika upendo?-Tuujenge mwili wa Kristo. Upendo huzidi yote, hata hiyo karama tuliyonayo-upendo ndio utakayoikuza, ikikosa upendo, inakwisha tu taratibu hivihivi. Wanadamu wengi tunateseka kwa sababu tumeshindwa kushirikishana karama zetu; Mjenge mwenzako kwa karama yako. Usikubuali ateseke ukiwa na karama yako hapo.

Kwenye somo la Injili, Yesu anashirikisha uwezo wake kwa huyu mama aliyekuwa akiomboleza kifo cha mwanaye. Anamfufua mtoto huyu. Nasi kama Yesu tutumie nguvu, uwezo na karama zetu kuwatuliza walio na huzuni kama huyu mama. Wapo wengi, tusipite tuache kuwatuliza, tutoe hata muda wetu tuwasalimu, itawatuliza.

Tusiwe wachoyo kiasi cha kuwaacha wengine waabakie katika huzuni kivyaovyao tu. Tuwe mstari wa mbele kwenye kushirikishana nasi tutafarijiana katika huzuni zetu.

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni