Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Septemba 05, 2022

Jumatatu, Septemba 5, 2022.
Juma la 23 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mt. Teresia wa Kalkuta, Bikira

1 Kor 5: 1-8;
Zab 5: 5-7, 12;
Lk 6: 6-11

WATU WASIO TIWA CHACHU!

“Mahusiano hayawezi kufa hivi hivi bila sababu. Yanakufa kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uelewa”. Kukiwa na upendo na uelewa uhusiano hauwezi kufa kamwe. Katika Injili ya Leo tunamsikia Yesu akimponya mtu aliye na mkono ulio pooza akiwa katika Sinagogi siku ya Sabato. Katika hali ya kukosa uelewa, kuwa na ubinafsi, na umimi wa viongozi wa Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo hawakuruhusu akili zao na mioyo yao kuelewa maneno na matendo ya Yesu. Walianza kumlaumu. Viongozi hawa walikuwa wanajali zaidi kushika sheria za Sabato zaidi ya kuleta nafuu kwa wanao teseka. Waliweza kuokoa mnyama aliyeanguka shimoni siku ya sababu zaidi ya kuonesha huruma kwa mwanadamu mwenzao.

Yesu alikuwa na haki ya kumuokoa yule mgonjwa sio tu kwa kumponya mkono wake lakini hata kumsamehe makosa yake na kumpa neema, Amani na furaha. Mt. Paulo anatuonya sisi tugeuze hali zetu, tuzirekebishe. Tuadhimishe uwepo wetu na Yesu, si kwakurudia chachu ya kale, chachu ya chuki na uovu bali tukiwa donge jipya lisilochachuka ambalo Paulo anasema ni weupe wa moyo na kweli. Tusiwe watu wasio eleweka katika maisha yetu ya ufuasi, tumgeukie Yesu kweli na tuweke lengo la kuacha maisha ya kale. Achana na kiburi, wivu, kushengenya wengine, kufurahia uovu, ubinafsi, uchoyo! Kwani hizi sio sifa za mfuasi wa Yesu. Tuombe neema ya Mungu ituongoze ili daima tuweze kufurahi jirani zetu wanapofanikiwa, tusiwazibie milango tusije tukawa kama mafarisayo na waandishi.

Sala:
Ee Bwana, tusaidie tuweze kusafisha chachu ya kale na kuiondoa, tunaomba utufanye donge jipya la uaminifu na kweli. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni