Jumamosi, Agosti 27, 2022
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Basi tafakari yetu inazidi kuongozwa kwanza na maneno matakatifu ya mtume Paulo kwa wakristo wa Korintho. Wakristo hawa basi kama tulivyokwisha kuona waliishi katika mazingira ya kusumbuliwa na wanafalsafa za ulimwengu.
Mji wa Korintho ulijaa wanafalsafa wengi na watu walioheshimika ni wale tu waliojua falsafa na kuwa na uwezo wa kujieleza kiufasaha. Waliokosa uwezo huu hawakuheshimika. Hivyo basi ili mtu kuweza kusoma falsafa hivi, ilibidi atokee familia yenye uwezo na hivyo basi maskini wote hawakuweza kusoma falsafa hivi. Ukristo ulikubali kila aina ya watu; haikuhangaika na falsafa au lile au lipi. Wao waliunganishwa na imani kwa Kristo, iwe maskini au fukara wote imani iliwaunganisha kwa Kristo.
Kutokana na hili, baadhi ya watu waliwadharau wakristo na kusema ni kikundi cha watu wasio na elimu, kinaruhusu kila aina ya watu, hata maskini ajiunge nao. Hivyo basi ilitokea kwamba baadhi ya wakristo wenyewe waliona aibu, na kuanza kukataa kujitambulisha na ukristo na kupendelea Zaidi vikundi vya wanafalsafa ili basi wapate heshima zaidi. Paulo anawaambia kwamba hili sio vyema. Falsafa za ulimwengu huu ni upumbavu machoni pa Mwenyezi, akili ya mwanadamu machoni pa Mungu ni ndogo sana. Hiki mwanadamu anachokiita hekima kwa kweli machoni pa Mungu ni ujinga mtupu.
Kumjua Kristo ndiyo hekima ya juu kuliko zote: na cha ajabu ni kwamba Mungu alianza kwa kuwachagua wale waliodhaifu machoni pa ulimwengu ili wajiunge na ukristo ili kuuridhishia ulimwengu kwamba hauna hekima; wanachokiita hekima kumbe ni upumbavu machoni pa Mungu.
Hekima yao imejikita kwenye kutafuta mali, cheo hata kwa kutumia dhuluma bila kutambua kwamba cha muhimu ni kuurithi ufalme wa milele. Hivyo wengi ulimwenguni hupambana na yale yasiyo ya msingi na kuacha ya msingi.
Hekima ya namna hii basi ndiyo inayosisitiziwa na Yesu katika injili. Anatoa mfano wa walikabidhiwa talanta kuonyesha kwamba kila mmoja basi anapaswa kuhakikisha kwamba anatumia muda na vipaji vyake kwenye kumzalishia Mungu ukuu na utukufu zaidi. Mungu hakutuumba tuache kutenga muda hata kidogo kwa ajili yake na watu wake. Hakutuumba ili tuishi kwa kudhulumu tu, au tufanye biashara kwa masaa yote tu, au tusome kwa masaa yote tu, au tulewe kwa masaa yote. Ipo nafasi yake. Nafasi aliyotupatia hii ndiyo itakayotupitisha kwenda kwake na ataidai.
Sisi tujiulize-hii nafasi tumeitumia vipi-lazima nikiangalia nyuma nione idadi kubwa ya watu niliowafanya wamjue Mungu kwa sababu ya mifano yangu na waliosaidiwa kwa sababu ya kujitoa kwangu-muda na rasilimali. Na hii ndio hekima inayozungumziwa na Paulo.
Wengi wetu tunafikiri kwamba hekima au ujanja unapatikana kwa watu maarufu kama wanamuziki na wacheza filamu maarufu. Hivyo hayo ndiyo maisha tunayoiga. Lakini kumbe ni upumbavu machoni pa Mungu.
Basi tumwombe Mungu atufundishe kuwa na hekima; ya kutumia muda na akili zetu kwa mambo ya msingi. Tunazitumia akili zetu kweli kufikiria mambo ambayo hayatatufikisha popote, unafikiria na kuliacha hapo tu. Hadi mwisho wa siku unaishia kujilaumu na kusema kumbe nilikuwa napoteza muda? Tutambue hekima ya kweli ni ipi na tutumie muda wetu vyema. Tumsifu Yesu Kristo
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Maoni
Ingia utoe maoni