Alhamisi, Juni 02, 2022
Ndugu zangu wapendwa, karibuni katika tafakari yetu ya leo. Bado tunaendelea kufurahia kipindi cha neema iletwayo na Roho wake Mungu kwa kipindi hiki cha Novena. Tuendelee kumwomba Mungu kwa kipindi hiki. Na leo katika tafakari ya neno la Bwana tukianza kwa kuiangalia injili yetu, leo tunamkuta Yesu akiendelea kuwaombea wanafunzi wake. Na cha zaidi ni kwamba anawaombea na wale watakaofuata nyuma ya wanafunzi wake. Anamuomba Mungu awashirikishe utukufu ule ambao atamshirikisha yeye pia.
Hapa ndugu zangu twapata maana ya kwa nini Yesu alituita rafiki. Yaani angalia anakuwa tayari kutuombea sisi makao ya kuwa pamoja naye pale Baba alipomwahidia. Hii ni heshima kubwa kwetu. Cha kumlipa ni sisi tupende utume wake. Yesu anataka injili yake na upendo wake umfikie kila mmoja ulimwenguni. Kila kiumbe chake kionyeshwe upendo. Kisiishi kwa kusumangwa bali kiufurahie ulimwengu; nacho kishirikishwwe rasilimali za ulimwengu, kisaidiwe ili kiweze kukuza vipaji vyake na kuvishirikisha ndani ya jamii, kikiugua kipendwe na kinaponyanyaswa atokee wa kumtetea. Sisi kama rafiki wa Yesu tuwe mstari wa mbele katika kutekeleza hili. Tumsaidie Yesu kama rafiki yetu ili lengo lake na nia yake hii iweze kufanikiwa na kuwafikia wote.
Kingine ni kwamba ndugu zangu kama Yesu anatuona rafiki kiasi cha kutushirikisha utukufu wake; yaani sisi kuwako pale alipo-sisi nasi tuwe tayari basi kuwashirikisha wengine utukufu wetu. Kuna baadhi yetu tuliojaliwa-lakini tunajifungia na kujitenga. Jaribu kuwashirikisha wengine hizo raha zako na furaha zako. Ukiwa hotelini ukiwa unakula nyama au divai yako na hapo kuna ombaomba anapita-usiache kumshirikisha utukufu wako. Mnunulie na yeye angalau hata maji basi afurahie huo utukufu. Ukiwa unapita njiani na gari yako halafu ukakutana na bibi kajitwika mzigo mzito usiache kumshirikisha kautufu kako. Washirikishe watu utukufu wako na Yesu atakushirikisha wa kwake.
Katika somo la kwanza tunamkuta Paulo sasa amekamatwa, yuko kizuizini. Amefanya kazi kubwa ya kuhubiri injili na watu wengi kawaokoa. Lakini sasa yuko kizuizini na bado Yesu hajampatia pumziko. Lakini Paulo cha ajabu ni kwamba bado anamatumaini ya ajabu. Anaona kama yote haya ni sehemu tu ya utume wake na hata hamlaumu Mungu au kumwomba amwondoe huko kizuizini. Anajitetea kama mtu wa kawaida tu. Paulo anayo mengi ya kutufunza. Kwenye utume au kwenye maisha ya kumfuata Kristo kuna shida zake na hivyo tujifunze kuziona kama sehemu ya utume wetu. Wengi wetu tunashindwa utume au kuishi kiaminifu maisha yetu kwa sababu hatujajifunza kuzipokea shida kama sehemu ya utume. Maisha ya Paulo yawe kwetu changamoto za kupambana na magumu ya kimaisha.
© Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Maoni
Ingia utoe maoni