Ijumaa, Mei 27, 2022
Ndugu zangu wapendwa, tafakari ya neno la Bwana leo inatupatia matumaini makubwa hasa kwa upande wa mitume wake.
Injili hii ni sehemu ya ule wosia ambao Yesu aliutoa muda mfupi kabla ya mateso na kifo chake. Yeye anawaeleza kwamba wakati utafika ambapo kweli watahuzunika na kuomboleza. Lakini wajue kwamba hili ombolezo litakuwa la muda tu kwani wakati wa furaha utakuja tena na wao watapata kufurahia tena. Anatoa mfano wa Mama anayejifungua mtoto; wakati wa kuzaa na wakati kabla ya kuzaa-huwa mateso yanakuwaga ni mengi na mama kweli huteseka. Lakini furaha inayokujaga baadaye kwa ajili ya kuzaliwa mtoto huwa inaondoaga uchungu wote. Anatumia mfano huu kwa wale mitume kwanza akimaanisha kwamba wao watalia na kuomboleza na kuwa katika masikitiko makubwa watakapomuona akiteswa msalabani. Lakini atakapofufuka, watakuwa na furaha kubwa kiasi kwamba hawatakumbuka yale mateso na uchungu walioupata.
Maana nyingine ya maneno haya ya Yesu ni kwamba kweli Yesu ataondoka kwao kwa kupaa mbinguni. Hapa kwa kweli watabakia wakifikiri kwamba wao ni wanyonge na wapweke. Lakini matunda ya Yesu kupaa mbinguni-yaani ujio wa Roho Mtakatifu unaotegemewa utasababisha matunda makubwa na furaha kubwa kwa hawa wanafunzi kiasi kwamba watausahau ule uchungu wote walioupata kwa kuondokewa na Yesu.
Halafu tukumbuke kwamba Yesu atakapokuja tena kwa mara ya pili, hawa wanafunzi nao watapewa jukumu la kuwahukumu mataifa kumi na mawili ya kabila la Israeli. Furaha watakayokuwa nayo kwa kipindi hiki itawafanya wasahau yale magumu yote waliyopitia enzi za utume wao wa duniani.
Haya ni maneno ya matumaini kwetu sisi wakristo.
Kwa kweli kila mmoja anaogopa shida na wakati wa uchungu. Kwa kweli ni wakati ambao ni mgumu, wakati mwingine hukupatia fedheha, utapata maumivu, utachekwa. Zote hizi ni shida na magumu ya wakati wa shida. Hivyo, kila mmoja anauogopa. Lakini nikuambie ndugu yangu, anaye endeleaga kupata shida ni yule anaye yakimbiaga magumu na kujitafutia raha zake na kuahirisha shida zake. Yule anayajidai kupata raha, anayeahirisha magumu ndiye anaye endeleaga kupata shida. Lakini yule anayepambana na magumu, anayejitosa katika magumu yote haya na kuyavamia bila kukata tamaa, akapambana nayo huyo anayamalizaga. Hivyo, anayepambana na mateso na kuteseka ndiye anaye yashindaga na kuja kupata raha.
Lakini anayeyakimbiaga na kuishi kwa raha, ndiye anayekujaga kuteseka. Mfano wale wanaokataaga shida za kusoma kwa bidii, labda kuamka mapema, kukimbizana na walimu na kuamua labda kutumia pesa zao za mikopo kula bata, kwenda disco chuoni na hivyo wanaishia kuwa na vitambi vikubwa, wanaanza kuitwa mabosi bila hata ya kumaliza degree-wengi wanaishiaga kufeli na kubakia katika kuteseka. Lakini wale wanaoteseka kuamka asubuhi kusoma, kutumia pesa zao kidogo za mikopo kujibana ili kununua vitabu na photocopy, wanaokosa hata fedha ya disco, wanaoishia kukonda kwa kujibana ili wasome na kudharauliwa hata na wenzao. Wao ndio wanaokujaga kuwa watu na kuitwa hata mabosi.
Hivyo ndugu zangu kuna mifano mingi lakini hii itufundishe faida iliyopo katika kupambana na mateso.
Katika somo la kwanza, tunamkuta Paulo anaendelea kuhubiri injili yake. Jana alikataliwa na Wayahudi na kujaribu kuwageukia watu wa mataifa. Leo Mungu anampatia matumaini kwamba asiogope kwani atazidi kuwa naye. Alipata matumaini haya baada ya yeye pia kuonesha nia ya kutokukata tamaa. Nasi ndugu zangu kamwe tusikate tamaa. Tusiogope kupambana na magumu. Ndani ya magumu kuna raha kubwa. Hakika ukishajiandaa kupambana na magumu, utamuona Mungu naye anakuja na kukupatia nguvu kama leo anapokuja na kumtia Paulo moyo. Tusichoke kupambana. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni