Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Mei 02, 2022

ASALI MUBASHARA-Jumatatu 02/05/2022

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana bado linazidi kutukumbusha juu ya habari njema tuliyoletewa na Pasaka yetu na katika injili, Yesu anatuendelea kutupatia fundisho ambalo kwa paska yetu hii kwa kweli linatufaa na tunaweza kulitumia na kusema kweli sasa tunaiishi pasaka na kweli tumefufuka na Kristo.

Yesu katika injili tunakutana naye kwamba, baada ya kuwalisha watu wengi mikate na kutaka ile siku kumfanya mfalme, sasa leo wanaendelearrèes kumtafuta lakini wanamtafuta wakifikiria kwamba atawapatia tena chakula. Hivyo hata lile lengo lao kutaka kumfanya mfalme ni kwamba walitaka ili labda awe akiwatengenezea chakula kwa mijuiza ili wao wale bila kufanya kazi. Sasa leo Yesu anatambua wanamtafuta kwa sababu ya chakula na si kwa kiu ya neno la Mungu. Naye anawaambia wazi lakini katika lugha nzuri na ya kiupendo bila kufoka au kuchukia. Anawaambia kwamba wanamtafuta kwa sababu wanatafuta kupewa tena chakula cha kimwili. Yeye anawaambia kwamba watafute chakula cha kiroho nao wanamwambia awaoneshe hicho chakula na yeye anasema chakula hicho ni kumwamini yeye.

Ndugu zangu, japokuwa wale makutano walikuwa wakimtafuta Yesu ili wapate chakula cha kimwili, tukumbuke kwamba uwepo wao pale karibu na Yesu uliwafanya angalau wafundishwe na kupatiwa chakula kifaacho. Ndivyo nasisi ndugu zangu; wengine tunaweza kwenda kanisani kujionesha tu, labda hata kuonesha mavazi au hata kuna wenye lengo la kutafuta waume au wake (hata kwa makanisa yasiyo ya kikatoliki watu wanaokwenda kanisani waweza kuwa na nia zao mbalimbali na za ajabu kama hizi). Lakini jua kwamba kitendo cha wewe kuwa pale kanisani, Yesu aweza kuongea na wewe na kubadili nia yako na kuchagua chakula bora kama makutano wanavyofanyiwa leo na Yesu. Lakini kama ungalikwenda maeneo kama ya bichi na mawazo kama hayo, hakika ungepotoka tu. hivyo, ndugu zangu, tujue kwamba kuhudhuria kanisani,au hata kushika vitu vitakatifu kama rozari, au picha kuziweka chumbani mwako au hata kuwa nazo kwenye gari-au kuwa katika maeneo matakatifu tu, maeneo ya sala-hata kama siku hiyo mawazo yako hayako katika kusali, jua kwamba Yesu aweza kukuokoa. Hivyo, tupende kukaa katika maeneo matakatifu Zaidi. Tambua kwamba ukiuawa-labda na ligaidi ukiwa ndani ya kanisa utaonekana kama shahidi lakini ukiuawa ndani ya nyumba ya muuza gongo –hata kama ulikuwa katika kusali-utaonekana kama ulikufa kama mlevi.

Katika somo la kwanza, tunaona mfano wa mtu aliyechagua chakula bora cha kumwamini Yesu. Lakini huku kumwamini kulimfanya achukiwe na watu kama tunavyoona katika somo la kwanza. Lakini yeye alizdi kumpenda Yesu. Nasi tujue kwamba tunapoacha labda njia za zamani na kutafuta chakula bora, twaweza kuchukiwa na wenzetu. Sisi tujipe moyo. Hakika tutashinda. Tumsifu Yesu Kristo.

©️ Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni