Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Aprili 24, 2022

Jiwe Kuu la Pembeni

“Jiwe walilolikataa waashi-limekuwa jiwe kuu la msingi, Zab 118:22.” Jiwe la msingi ni jiwe muhimu sana katika jengo. Mara nyingi huwekwa na kiongozi maalumu.

Jengo zima huchota sifa yake toka kwa jiwe hilo. Msemo huu ulitumika katika Israeli pale mtu anayedharauliwa anaponyanyuka na kuwa mtu muhimu. Yesu ndiye jiwe lililokataliwa, likatukanwa, likatemewa mate; lakini mwishowe amefufuka, amekweza juu kuliko yote. Na ambaye hatajenga juu yake hakika hatadumu. Yeye ni matumaini ya dunia yote. Katika somo la kwanza, wakristo wa mwanzo wanaamua kujenga juu ya Yesu. Kwa nguvu ya jina la Yesu, waliweza kufanya mengi, walifanya miujiza mingi na kuwafariji wengi katika jamii. Ukijenga kwa Yesu tunapata ushindi.

Katika somo la pili, tunaelezwa juu ya mamlaka ya Yesu. Anaonekana katikati ya vinara saba vya dhahabu kuashiria kwamba yeye ndiye kichwa na nguzo ya kanisa; yeye ndiye mwenye kuyashika makanisa yote mikononi mwake-bila yeye hakuna kanisa. Macho yake ni kama mwali wa moto kumaanisha kwamba alikuwa na ufahamu wa kila kitu. Yeye ni wa kwanza na wa mwisho; alikuwa amedhaniwa kufa lakini sasa anaishi. Tusione shaka kumwungama Yesu kwani yeye anaishi milele.

Katika somo la injili, Yesu anawatangazia wanafunzi wake amani. Anawavuvia roho atakayewawezesha kuondoa dhambi za ulimwengu. Hapa twatambua ukuu wa huruma ya Mungu. Wanadamu wanahitaji msamaha wa dhambi zao na hivyo mitume wanakabidhiwa mamlaka ya kuwaondolea watu dhambi.

Tunaalikwa leo tuikimbilie huruma ya Mungu. Thomaso anauonja kwa namna ya pekee na kwa undani kabisa upendo wa Yesu na huruma yake. Sisi tuikimbilie huruma hii. Majeraha ya Yesu ndiyo njia pekee kuelekea katika moyo wake.

Moyo wa Yesu hutoa uponyaji. Thomaso alikutana na moyo huu ukamponya na kumwondolea mashaka yake yote. Nasi tunaalikwa kukutana na moyo wa Yesu leo na kubadilika.
Thomaso alipoteza karibu wiki nzima bila kumwamini Yesu. Sisi tuombe ili tusije tukapoteza maisha yetu yote bila kumwamini Yesu. Kutana na Yesu mfufuka leo. Wapo ambao bado hatujakutana naye.

Tumwangukie Yesu wetu. Tumkubali abadili maisha yetu. Ukubali atembee nawe akuondolee na mashaka yako yote. Akupe amani. Amani inaanza kwa kukusamehe na kusamehewa, baada ya Simoni Petro kusamehewa-ndipo alipopata amani. Msamaha ndio ufunguo wa mafanikio yote. Mwambie Yesu akusamehe leo.

Sala:
Bwana wa huruma, nisaidie leo niweze kuelewa maana ya huruma yako, nisaidie na mimi pia niweze kuwa mjumbe wa huruma hiyo,
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni