Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Aprili 27, 2022

Jumatano, Aprili 27, 2022.
Juma la 2 la Pasaka

Mdo 5:17-26
Zab 34:2-9
Yn 3:16-21


KUVUTWA KWENYE MWANGA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo, neno la Bwana katika somo la injili linazidi kutuelewesha juu ya upendo aliotuonesha Yesu kwa kipindi hiki cha pasaka; Yesu anapozungumza na Nikodemo katika Injili leo, anamuonesha dhahiri kwamba yeye ni nani na nini alichokuja kuutendea ulimwengu. Yeye leo anasema moja kwa moja kwamba amekuja ili ulimwengu usipate kupotea bali uwe na uzima wa milele na ukweli huu umedhihirika hasa kwa kipindi hiki cha Pasaka ambapo tumeshuhudia upendo mkubwa sana toka kwa Yesu. Yesu anamweleza Nikodemo juu ya upendo huu mkubwa lakini pia anatoa masikitiko yake kwamba watu wamekataa kuuona upendo huu na kutamani giza zaidi ya upendo huu, na kuona kwamba ni afadhali kubakia katika utumwani, kubakia katika dhambi kama baadhi ya wana wa Israeli walivyotamani kurudi utumwani Misri au utumwani Babuloni baada ya kukombolewa.
Katika somo la la kwanza, tunaona kwamba viongozi wa Kiyahudi ndio watu wa kwanza wanaokuwa wa kwanza kutamani giza kwa kukataa habari njema itangazwe na hivyo waliukataa mwanga ulioletwa na Yesu na hivyo ni kama vile wanakuwa kama wale Wayahudi waliotamani kurudi Misri. Mitume wanakuwa watu wa kwanza kutamani habari njema itangazwe na hivyo waliupokea mwanga na wanakuwa kama wale Wayahudi waliotamani kwenda katika nchi ya ahadi na kukataa kurudi Misri na hivyo wanakuwa tayari kuvumilia shida zote.
Biblia inatuambia kwamba wale waliokataa kuvumilia kusafiri kwenda katika nchi ya ahadi na kuamua kuanza kurudi misri waliishia kufa njiani kwani njia yao haikuwa na ile nguzo ya moto. Lakini wale waliovumilia na kusonga mbele waliishia mikono salama kwani njia yao ilikuwa na ile nguzo ya moto usiku na wingu mchana. Ndicho kinachoonekana kwa wale mitume leo. Wao wamechagua njia ya mwanga, kumfuata Kristo na kukataa utumwa wa shetani na hivyo wanavumilia shida na taabu. Na kwa kweli watashinda kwani njia yao ipo mikononi mwa Bwana. Lakini kwa wale waliochagua giza na kuamua kumkataa Yesu asitangazwe, yaani hawa viongozi wa Kiyahudi, wataishia kushindwa kwani njia yao haiko na Bwana. Watakufa njiani kama baadhi ya wale wana wa Israeli ilivyokuwa.
Tafakari hii ndugu zangu itufunze tutambue kwamba mambo ya Bwana yanahitaji uvumilivu. Kama Waisraeli walivyovumilia kule jangwani, nasi yatupasa kuvumilia katika maisha yetu ya kiimani. Halafu kingine tuepuke kuwadhulumu watu. Mitume leo wanadhulumiwa lakini Bwana anawatendea mambo makubwa na kuwa upande wao na kuwaokoa. Nasi tutambue kwamba tunapowadhulumu watu, kamwe hatutafanikiwa kuwaangusha kwani Bwana huzidi kuwa nao na wakimlilia Bwana kama zaburi yetu ya wimbo wa katikati inavyotuambia hakika tutaumbuka vibaya sana. Hivyo, tuombe msamaha kwa wale tuliowadhulumu.Tutambue kwamba wengi kati yetu tumeadhibiwa na Bwana kwa sababu tunadhulumu watu. Ukidhulumu kamwe hufanikiwi.

Maoni


Ingia utoe maoni