Jumamosi, Aprili 09, 2022
Jumamosi, Aprili 9, 2022,
Juma la 5 la Kwaresima
Ez 37: 21-28;
Yer 31: 10-13;
Yn 11: 45-56
KUJITAZAMA KIDOGO NA KUMTAZAMA YESU ZAIDI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana kabla ya kutuingiza katika juma kuu tutasikia juu ya mwongezeko wa hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na baadhi ya viongozi wa Kiyahudi. Mipango ya kutaka kumwangamiza bado inazidi kupangwa kila siku na leo basi inaonekana dhahiri kwamba hakika hawa watu watamteketeza. Lakini Yesu tayari amekwisha kaza moyo wake kama gumegume na hakika kamwe hataogopeshwa na kelele za hawa watu bali atazidi kuwa mwaminifu na mwishowe atatoa maisha yake kama fidia na ukombozi wa wengi.
Kanisa leo limepangilia masomo yake kwa ajili ya kututafakarisha kutafakari namna jinsi Yesu anavyojiandaa kutolewa kama sadaka isiyokuwa na waa na namna anavyoitoa kwa upendo. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Ezekieli tunakutana na Mungu akitoa habari za ukombozi kwa taifa la Israeli. Kipindi hiki waisraeli wapo utumwani Babuloni na wamekwisha onja machungu ya utumwa. Sasa Mungu anamwagiza nabii huyu kutoa ujumbe wa kiukombozi kwamba Bwana anawapenda, azijua shida zao na kamwe hatawaacha atakuja kuwatoa katika utumwa wa shida zao. Katika Injili, tunakutana na mwendelezo wa historia kama hii hii ambapo sasa naye Yesu amekwisha jiandaa kweli kufa na Kayafa anatabiri (bila hata ya kufahamu undani wa anachotabiri) kwamba yafaa mmoja afe kwa ajili ya taifa nzima lisiangamie. Sasa Yesu amekwisha jiandaa kufa. Lakini kufa huku kwa kweli ni Yesu kujitolea. Yeye anakufa baada ya kutenda matendo mema, bila kosa, baada ya kuwatendea watu miujiza mingi na mikubwa sana. Kila mmoja anapaswa kumshukuru Mungu kwa ajili ya upendo huu kwetu.
Nasi ndugu zangu tunaalikwa kufanya kama Yesu alivyofanya hasa katika kipindi chetu hiki cha juma kuu. Yeye alilipwa baya badala ya wema, alipokuwa anatenda mema kumbe watu wengine wanampangia mabaya. Nasi mambo kama haya yatatupata. Kuna watu wanaogopa watenda mema-wanataka mtenda dhambi kama wao ili mambo yao yasijulikane, wakisikia unawapa changamoto katika suala la sala, uaminifu hawataki, watatafuta njia ya kukufundisha mabaya tu. Ndivyo baadhi ya viongozi wa dini ya Kiyahudi walivyomtaka Yesu awe na walivyoshindwa wakamuua. Lakini tukumbuke kwamba Yesu angekubaliana kuwa mtu mdhambi kama wao, hakika naye asingeweza kuwa mkombozi. Nawe tambua kwamba kama utajiunga na wadhambi au kutimiza matakwa yao, hakika hutaweza kuiletea dunia au jumuiya ukombozi. Tumwige Yesu ndugu zangu leo. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni