Jumapili, Aprili 10, 2022
JUMAPILI YA MATAWI MWAKA C 10/04/2022
------------------------------------------------
Hossana Mwana wa Daudi
Katika Liturjia ya leo, tunakumbwa na hisia mbili tofauti. Tunaanza liturjia yetu kwa utukufu na shangwe kuenzi jinsi Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe kwa kuimba ‘hosanna, hosanna juu mbinguni.’ Watu walifurahi kumuona Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe, lakini hali hii inaanza kupotea taratibu; baada ya kuanza kuingia kwa undani katika masomo yetu, hali inabadilika na kuwa ya kushtua na huzuni.
Injili inaishia na kutundikwa kwa Yesu msalabani na Yesu analia kwa sauti kuu na kusema “Mungu wangu Mungu wangu, mbona umeniacha” na baada ya hayo, Yesu anatoa pumzi yake ya mwisho na kukata roho.
Ni nini kilitokea kwa watu ambao walikuwa wakishangilia na kumsifu alivyokuwa anaingia Yerusalemu? Hawa ni watu wa umati geugeu wenye tabia za kushabikia mambo fulani fulani. Huu umati ulimuacha Yesu kipindi cha mateso na kipindi alipokuwa msalabani.
Huu ndio wakati aliowahitaji zaidi lakini wao walimuacha. Kuna kipindi Yesu anakuhitaji zaidi. Yesu anakuhitaji katika maskini, yatima na wagonjwa tunaokutana nao kila siku. Yesu anakuhitaji umwendee umwabudu katika Ekaristi na kutoa mfano kwa kizazi kijacho kwa matendo yako mema. Tutambue kwamba Bwana Yesu ndiye atakayetupatia hadhi.
Yule punda aliyembeba Yesu, alipokuwa amembeba, punda aliheshimika, akatembea juu ya nguo za watu, hakuna aliyempiga. Lakini alipokuwa anarudishwa nyumbani kwa mmiliki wake, hakupokea heshima kama ile ya mwanzo. Sisi tusimuache Yesu.
Katika historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, ni Mama Bikira Maria pamoja na mtume mwaminifu kama Yohane na wengine wachache ndio walioweza kusimama karibu na Yesu. Wengi kati ya Wafuasi walimkimbia. Upo wakati na sisi tutakimbiwa na marafiki zetu pia. Tunapaswa kumtumainia Bwana Yesu.
Umati uliomshangilia Yesu mwishowe uliishia kumpenda Baraba kuliko Yesu. Je, mimi ni Mkristo wa makundi tu au Mkristo tu tukiwa wengi? Je mimi ni Mkristo tu pale ninapopata pato fulani au sifa fulani? Wengi ni wakristo wa makundi na yafaa tubadilike. Petro alisikia jogoo akiwika na kulia na kutubu. Dunia yetu inapaswa kuiga mfano wa Petro-ikubali kutubu. Mateso ya Yesu yalileta wema hata kwa wale adui zake. Pilato na Herode walirudisha urafiki na Yesu alimponya mtumishi wa kuhani mkuu aliyekatwa sikio na Petro. Mateso ya Yesu yanapaswa yawe chanzo cha uponyaji kwetu na kwa wenzetu.
Sala:
Bwana, ninapojaribiwa, naomba unipe matumaini. Ninaomba juma hili kuu, libadilishe nyakati zangu za giza,
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni