Jumapili, Aprili 03, 2022
*DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA 03/04/2022*
*USITENDE DHAMBI TENA*
Yesu anatuambia kama alivyomwambia yule mama aliyefumaniwa katika uzinzi:“hata mimi sikuhukumu, nenda lakini usitende dhambi tena.”
Yesu anajua kwamba sisi ni wadhambi-lakini anatupatia muda wa kujirekebisha, hata pale wenzetu wote wanapotaka tuadhibiwe. Yesu anatutaka tusitende dhambi tena. Yawezekana ikawa matendo yako yamekutenganisha na wenzako na hakuna anayetamani kuishi na wewe. Lakini kwa Bwana bado unabakia kuwa wa thamani kubwa. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu anayetupatia muda wa kujirudi. Tujifunze kutumia vipindi atupatiavyo kujirekebisha.
Nasi tuwe tayari kuwaelewa wenzetu na kuwapatia nafasi ya kutubu.
Zaburi ya wimbo wa katikati toka Zaburi ya 126 inatusisitizia: “Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi.” Zaburi hii iliimbwa kila mwaka wakati Wayahudi waliokuwa wanaishi kwenye mataifa mbalimbali walipokuwa wanapanda na kuja Yerusalemu kwa ajili ya kusheherekea Pasaka.
Ni Zaburi yenye kuashiria ukombozi uliowahi kufanywa na Mungu kwa wana wa Israeli tangu alipowavusha bahari ya shamu na baadaye kuwatoa utumwani Babuloni. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliye chanzo cha ukombozi wote. Yeye hutupatia muda wa kutubu na huruma yake ni kuu. Nabii Isaya katika somo la kwanza anashangilia huruma na ukombozi toka kwa Mungu wetu. Mwenyezi Mungu kufanya maajabu; kufanya njia hata pale pasipopitika.
Alitengeneza barabara katikati ya bahari na kufanya vijito vya maji jangwani kwa ajili ya taifa lake teule. Yeye astahili kuheshimiwa na mataifa yote. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Upo wakati unafika na sisi tunajiona kana kwamba hatuna njia, tunashindwa kusonga mbele.
Mwenyezi Mungu aweza kutufungulia njia. Siku ya leo tumweleze Mungu ni njia zipi za kwetu zilizozibwa, ili azifungue. Tunapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu atufungulie njia kama alivyowafungulia Waisraeli jangwani.
Yesu anaonesha ukamilifu wa huruma ya Mungu pale anapotangaza msamaha kwa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi.
Yesu alimtaka mama huyu akatumie kipindi kilichobakia kujirekebisha. Hii ni mojawapo ya sehemu katika injili yenye kutoa mguso mkubwa kwa watu juu ya huruma ya Yesu. Jibu lake ni la kimungu kwamba Mwenyezi Mungu hutoa nafasi kwa mwanadamu. Mungu hafurahii kifo cha mtu mwovu bali auache mwenendo wake mbaya apate kuishi. Bwana Yesu anaielewa hali ya wanadamu.
Sisi tunapaswa kuwa waelewa wa wenzetu pia. Ulimwenguni hawaishi malaika. Hivyo tujifunze kuwapokea wenzetu kama zawadi. Wapo pia baadhi ya wenzetu wanaopakwa matope kwa dhambi ambazo hawajawahi kutenda. Siku ya leo pia tunaalikwa kuangalia ni mawe gani tuliyoyabeba tupate kuwapiga wenzetu.
Mawe yetu yaweza kuwa ni midomo yetu michafu yenye kutangaza dhambi za wenzetu au yenye kusema siri za wenzetu. Tukubali kurudisha haya mawe chini. Mawe haya yatatuzuia kuingia kwenye ufalme wa Mwenyezi Mungu.
Sala: Bwana, wewe ni ufufuo na uzima. Nisaidie niweze kutambua uzima wa Kimungu ndani mwangu,
Amina.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Maoni
Ingia utoe maoni