Jumanne, Machi 29, 2022
Jumanne, Machi 29, 2022
Juma la 4 la Kwaresima
Ez 47: 1-9, 12;
Zab 46: 2-3, 5-6, 8-9;
Yn 5: 1-16.
INUKA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Mungu katika kipindi hiki chetu cha Kwaresma inaanza kutuvuta kuelekea kwenye fumbo la wokovu wetu. Kuanzia siku ya leo, Injili yetu itaanza kuonesha hali ya kutokuelewana kati ya Yesu na wakuu wa Kiyahudi. Yesu ataanza kuwaeleza ukweli na atafanya matendo makuu ya Mungu bila kuogopa macho au nguvu zao. Kwa sababu hiyo, wakuu wa Kiyahudi watakasirika na wataanza kutafuta namna ya kumuua tu. kwa mfano, katika somo la Injili Yesu anamponya mgonjwa aliyekuwa ametelekezwa karibu na bwawa lililokuwa linaaminika kutoa uponyaji.
Huyu bwana alikaa karibu ya hilo bwawa miaka na miaka akisubiria mtu wa kumdumbukiza huko ili aponywe lakini hakuna aliyemhurumia. Makuhani, waandishi na wakuu wote wa kidini wa Kiyahudi hawakujihangaisha na mateso yao. Yesu kwa bahati leo anapita na kumuona na kumponya lakini badala ya hili kuleta furaha, linaleta fujo kwa sababu kaponywa siku ya sabato na wale viongozi wataanza kumtafuta Yesu ili wamuue.
Lakini kadiiri tutakavyosikia katika injili yetu kuanzia leo hii, Yesu atazidi kuwaeleza ukweli na wao watazidi kuchukia na Yesu hataogopa na mwishowe atakufa na akiutetea ukweli na kutuletea ushindi na ukombozi.
Ndugu zangu, tunapoanza kusikia masomo ya namna hii, tufurahi tukijua kwamba Yesu sasa kakaza moyo wake kama gumegume-haogopi na yeye kasema lazima atuokoe na hii itakamilika ile siku ya ijumaa kuu na ile siku ya pasaka. Na hata katika somo letu la kwanza leo, tunasikia nabii Ezekieli akielezea juu ya ukombozi utakaotoka kwa Mungu. Anaufananisha wokovu huu na maji yanayotoka chini ya altare ya hekalu la Yerusalemu.
Maji haya yalianza kama chemchemi ndogo lakini kadiri umbali ulivyozidi kuongezeka, yalizidi na kuwa mto mkubwa. Zaidi, maji haya yalileta uhai kila yalipopitia. Miti iliota na ndege wa angani kuongezeka kila mahali yalipopitia.
Somo hili linatoa ujumbe kwetu kwamba Yesu anatuletea ukombozi na hizi ni habari njema. Sisi ndio wa kuutangaza wokovu huu na kuufanya ukue na kufika mbali Zaidi na kule ulikoanzia.
Hivyo ndugu zangu, leo injili imeanza kutueleza kwamba Yesu kakaza macho yake kama gumegume kuhakikisha kwamba anatuokoa. Nasi tuupeleke huu wokovu kwa wengine kama somo la kwanza lituambiavyo. Tujitahidi kuwa Yesu popote tulipo. Tuzidishe matendo ya huruma na kufunga. Nisiwe na hasira na wenzangu leo au kuwachukia bure. Nitoe msamaha kwa wadeni wangu kadiri iwezekanavyo, niwe mtu wa sala Zaidi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni