Jumatatu, Machi 28, 2022
Jumatatu, Machi 28, 2022
Juma la 4 la Kwaresima
Isa 65: 17-21;
Zab 29: 2, 4-6, 11-13;
Yn 4: 43-54.
IMANI KWA YESU
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya Neno la Bwana katika asubuhi hii tuanze kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo nabii Isaya anasisitiza kwamba amekuja kufanya mbingu na dunia mpya. Mambo ya kale hayatakumbukwa. Haya yalikuwa ni maneno ya matumaini kwa wana wa Yuda kwa sababu mambo ya kale kwa hili taifa la Yuda yalikuwa ni ya kusikitisha. Historia ya zamani iliwakumbushia maumivu ya utumwa wa Babuloni, adhabu mbalimbali kama njaa, kugandamizwa na mataifa mengine, uchungu wa kukaa bila hekalu, uonevu na dhambi za kila aina.
Sasa nabii anawapatia matumaini hawa wa Yerusalemu akiwaambia kwamba kutakuwepo na upya na historia mbovu ya ukale haitakumbukwa tena. Ndugu zangu, ujio wa Yesu ulikamilisha huu upya wote uliotabiriwa na nabii Isaya. Yesu ndiye mwenye kutuhurumia na huwa hakumbukagi ya kale bali hutuletea upya. Katika injili yetu ya leo, tunasikia jinsi anavyomponya huyu mtumishi wa akida wa kirumi. Hapa yamaanisha kwamba Yesu huangalia yote katika upya, haangaiki kutazama historia au cheo cha mtu au ubora wa mtu. Leo anamponya mjakazi tena wa mpagani. Hii yamaanisha upendo Mungu alionao kwa kila mtu.
Sisi tunaalikwa kuiga upendo huu. Tuwe tayari kumhudumia kila mtu na kutoa misaada yangu. Wakati wa kutoa msaada, nisiangalie kabila, urafiki, dini au elimu. Nisaidie kila mtu, vikundi vyetu mbalimbali tunavyoviunda pia viwe na lengo la kuwasaidia kila mtu. Tusijidai kujiunga watu wa kabila Fulani Fulani au maeneo Fulani Fulani na kusadiana na kuwaacha wengine wakiteseka. Hapa tutakuwa hatumpendezi Mungu, tutakuwa tunafanya upagani. Tuwe tayari kuungana na kusadia wote. Nisifungwe na eneo au kabila. Kristo angechagua eneo au kabila Fulani basi sote tungeishia motoni. Sisi tumwige-tusifungamane na kabila au eneo Fulani. Kristo anapomponya huyu mjakazi atuamshe ili tuache ubinafsi na utengano. Wengi wamekufa mahospitalinI au kushindwa hata kusoma kwa sababu tunafikiri kwamba ndugu ni yule tu tulietoka naye eneo moja au tuliyezaliwa naye na hivyo wengine hata kama wana uwezo wanashidwa kusoma na sasa wamezubaa huko tu labda wanavuta bangi na kula dawa za kulevya. Tusikubali kuwa na historia mbaya ya kushindwa kuwasaidia binadamu wenzetu
Maoni
Ingia utoe maoni