Jumapili, Machi 27, 2022
DOMINIKA YA 4 YA KWARESIMA MWAKA C
KUMRUDIA MUNGU!
Katika mfano wa Mwana mpotevu tunaona ujasiri wa huyu Mwana kwa kuchagua kurudi kwa Baba yake. Ni kweli, alitambua udhaifu wake na akaamua kurudi kwa Baba yake kuomba msamaha na kumuomba amfanye kama mmoja wa wafanyakazi wake. Alifanikiwa kurudi.! Swali la kujibu “kwanini?”
Ni vyema kusema kwamba huyu mtoto alirudi kwa Baba yake, kwanza kabisa kwasababu alitambua kutoka moyoni mwake tabia ya Baba yake. Baba alikuwa Baba mwema. Alionyesha kujali na kuwa na upendo kwa mtoto daima katika maisha yake. Ingawaje mtoto alimkimbia Baba yake, haikubadilisha ukweli kwamba yeye alitambua kuwa Baba yake alikuwa mtu mwema na kwamba anampenda. Pengine hakutambua ni kwa jinsi ghani, hadi alipo tambua mwenyewe. Ni wazi kwamba ni kwasababu ya utambuzi huu kutoka moyoni mwake unaompa ujasiri wa kurudi kwa Baba kwa matumaini ya upendo wa Baba yake.
Hili linafunua kuwa, upendo wa kweli unafanya kazi. Daima unafanya kazi. Hata kama mtu akikataa upendo mtakatifu tunaompa, lazima daima una ongeza kitu katika maisha yao. Upendo wa kweli usio na masharti ni vigumu kuukataa na kuutupilia mbali. Mwana mpotevu alitambua hili, na sisi pia tunapaswa kuwa hivyo. Huu ndio upendo alionao Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mtu. Yeye sio Mungu mkali na mgumu. Ni Mungu anayependa kuturudisha kwake na kutupatanisha naye. Anafurahi tunapo mrudia na kuomba mahitaji yetu kwake. Ingawaje tuna wasi wasi, yeye hana wasi wasi kwa upendo wake, daima anatusubiri sisi, na sisi wenyewe kutoka ndani kabisa tunatambua hilo.
Kwaresima ni kipindi kizuri sana kwa sakramenti ya kitubio. Na sakramenti hiyo ndio ujumbe wote katika mfano huu. Ni mfano wa sisi kwenda kwa Baba yetu na dhambi zetu na atatupokea kwa huruma. Inaweza kuogopesha na kuwa na wasi wasi kwenda kwenye sakramenti ya kitubio, lakini tukiingia katika sakramenti hiyo kwa uaminifu na katika kweli, tunaona furaha tunayopata na Amani kuu. Tunajisikia Amani na kuacha mizigo iliyo tuelemea rohoni. Mungu, anatukimbilia, na kunyanyua mizigo yetu na kuitupa nyuma yetu. Usikubali kipindi hichi cha kwaresima kipite bila kuungama! Hakuna na tena, wala hakuna sehemu nyingine waweza kupata furaha hii ya kuunganika na Mungu katika kweli. Usijioneee huruma kwa kujibembeleza kwamba nitamweleza tu Mungu mwenyewe nikiwa chumbani kwangu. Nenda kaungame katika hali ya uaminifu na kweli kadiri ya Imani yetu. Mungu anakusubiri. Usikubali kubaki katika gereza la dhambi. Fanya uamuzi kama Mwana mpotevu.
Somo la Pili linatueleza kwamba tunapo amua kukaa ndani ya Kristo yakale yanaisha na tunakuwa wapya. Nikweli hatuwezi kumchanganya Kristo na hali yetu ya dhambi. Tunapo amua kumfuata basi yeye anatufanya sisi kuwa wapya na kumtumikia tukiwa viumbe vipya. Hata kama ulikuwa umetenda dhambi kubwa namna gani, wewe unakuwa kiumbe kipya, na kamwe mtu asikutambulishe kwa dhambi zako za zamani! Kama Mt. Paulo alivyompokea Yesu, yeye alikuwa kiumbe kipya na wala yazamani hayakumzuia tena kutekeleza ujumbe wa Yesu.
Turudi kwa Baba yetu yeye atattufikisha Mbinguni kama alivyo wafikisha wana wa Israeli katika nchi ya ahadi na kufirahia maisha!. AMINA.
Maoni
Ingia utoe maoni