Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Machi 25, 2022

Ijumaa, Machi 25, 2022,
Juma la 3 la kwaresima

Sherehe ya Kupashwa habari ya kuzaliwa Bwana

Isa 7:10-14, 8:10;
Zab 40:7-11;
Ebr 10:4-10;
Lk 1:26-38

Ndugu zangu wapendwa, leo ni sherehe ya kupashwa Bikira Maria habari kwamba atapokea mimba na kumzaa Mkombozi wa ulimwengu. Bikira Maria anapashwa habari na Malaika na kwa kitendo chake cha kukubali leo, Mwana wa Mungu anaanza kutungwa mimba katika tumbo la Mama Maria. Huyu mwana ndiye ukamilifu wa historia ya wokovu, ndiye sababu ya ulimwengu kubarikiwa, ndiye aliyefuta laana iliyoletwa na dhambi ya wazazi wetu wa Mwanzo.

Ulimwengu ulipata mwanga kwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Ulimwengu ulivyokuwa kabla ya kuzaliwa Yesu na baada ya kuzaliwa Yesu ni tofauti.
Kwa jibu moja la utii, kwa jibu la ndio lililotolewa na Bikira Maria lilikuwa sababu ya ulimwengu kupata baraka kubwa. Mungu hufanya kazi pamoja na wenye utii. Mfalme Sauli alikosa utii akapoteza ufalme wake-licha ya kuwa na nia ya kutaka kumfanyia Bwana tendo jema la kumtolea sadaka; mke wa Lutu alikosa utii kwa sauti ya Mungu na kugeuka kuwa mnara wa chumvi, Musa katika maji ya Meriba alikosa utii kwa sauti ya Mungu na kupata adhabu ya kwamba hataiona nchi ya ahadi. Abrahamu aliitii sauti ya Mungu na kuuletea ulimwengu baraka kubwa. Mama Maria anakuwa kilele cha utii wenye faida kubwa-yeye kwa jibu lake la ndio-ulimwengu unapata faida kubwa.

Ndugu zangu, utii ni bora kuliko sadaka za aina yoyote ile. Sisi tusiache kuwa watii. Tutambue kwamba ulimwengu unakosa mengi, unakosa viongozi bora, unakosa manabii, watumishi wa kutosha na watu watakatifu kwa sababu ya kiburi, tunakataa kushirikiana na Bwana. Ni wachache wenye utayari wa kusema kama Maria kwamba mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama nilivyonena. Mama Maria atufunze utii.

Tuwe na utayari wa kuitii sauti ya Bwana pia moyoni mwako. Kila mmoja wetu ajichunguze ni namna gani ameshindwa kutekeleza utume wake kwa sababu ya kiburi chake, kiburi kama cha yule mwana mpotevu. Leo tujizatiti na kurudi kwa Baba kama yule mwana mpotevu na hakika atatupokea. Hakuna sadaka iliyo kuu kama utii.

Tutambue kwamba jibu letu kama wakristo ni lazima liwe mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyonena. Ni lazima tujiandae kutoa neno la namna hii maishani mwetu-upo wakati utakaofika ambao sisi hili neno la Maria lazima liwe ndio jibu letu-labda kwenye magonjwa yetu, uzee wetu na changamoto mbalimbali.

Tukishindwa katika hili, tutaishia kuishi kinyume cha ukristo wetu. Tujitahidi. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni