Jumatano, Machi 23, 2022
Jumatano, Machi 23, 2022.
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa
Kumb 4:1, 5-9
Zab 147: 12-13,15-16,19-20;
Mt 5:17-19
YESU: UTIMILIFU WA SHERIA
Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linazungumzia juu ya sheria ya Bwana. Hii ni takatifu, yenye uwezo wa kumtia mjinga hekima, ukiishika unachanua, unangaa, unakuwa na mvuto, unanukia kama mchungaji na hivyo kondoo wanakufuata.
Asiyeishika sheria ya Bwana huchakaa. Mchungaji asiyeishika sheria ya Bwana hushindwa kuwavutia kondoo.
Katika somo la kwanza, Musa anawaeleza waziwazi wana wa Israeli kwamba ushikaji wa amri za Bwana ndio utakaowawezesha kuingia katika nchi ya ahadi na kuimiliki. Pia utawafanya waheshimiwe na watu wa mataifa mengine, na pia utamfanya Bwana Mungu wa Israeli aheshimiwe na watu wote wa ulimwengu.
Haya yote yatatokana na jambo moja la utiifu kwa sheria ya Mungu. Hivyo Israeli anaambiwa awe mtu wa kukumbuka matendo ya Mungu; asiwe wa kusahausahau na awe wa kuyasimulia matendo yote anayoyaona kwa kizazi kijacho. Wasisahau hata kimoja walichotendewa na Bwana. Wasiwe watu wa dharau, kila wanachokiona wakiheshimu, kila muujiza wanaotendewa waubebe kwa umakini. Wasiwe watu wa kusahausahau, na waueleze kwa vizazi vijavyo.
Huu ndio ujumbe tunaoambiwa na sisi tuuchukue ndugu zangu. Dharau na kutojali na kusahau mapema zimeiharibu imani yetu. Tunapoonesha dharau kwa mambo matakatifu, kwa watumishi wa Mungu, na kuwa watu wa kusahau haraka ndio sababu za imani yetu kupotea. Kama tunataka kuendelea kiroho ni lazima tuhakikishe kwamba mambo matakatifu, na matendo makuu ya Mungu-yanapewa nafasi ya pekee kila siku, nisikaribishe aina yoyote ile ya kutojali katika mambo matakatifu.
Pia tusiwe watu wa kusahau mapema.
Yesu katika injiili anasisitiza kwamba yeye alikuja kuikamilisha sheria ya manabii na kamwe hakuja kuiondoa. Sheria ya Bwana ndiyo inayotufanya tungae, tuweze kucheka, kukaa na amani na wenzako. Pia ndiyo inayotufanya tuheshimiwe, tuwavutie na kondoo kuja kwetu. Hivyo tushike sheria na viapo vyetu.
Wengine baadhi yetu tunalalamika, tunaweza kusema kwamba tumeonewa na kunyanyaswa lakini tukijichunguza kiundani ni kwamba hatukuzishika sheria za Bwana, na pia tusipozishika sheria za Bwana tunachukiza, hatupendezi, hatutamaniki.
Anayezishika sheria za Bwana hata kama ana sura mbaya-atavutia tu. Binti asiyeshika sheria za Bwana-hata kama ni mzuri kiasi gani-atakosa mvuto tu. Sisi tuziheshimu sheria za Bwana.
Maoni
Ingia utoe maoni