Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Machi 20, 2022

Machi 20, 2022.
------------------------------------------------
Domika ya 3 ya Kwaresima

Somo 1:
Kut 3:1-8, 13-15 Tunaona Mungu anaongea na Musa katika kichaka kinachowaka moto bila kuteketea na anamwambia awaongoze watu wa Israeli kutoka katika Inchi ya Misri.

Wimbo wa katikati: Zab 103: 1-4, 6-8, 11 “Bwana amejaa Huruma na Neema”

Somo la 2:
1Kor 10:1-6, 10-12 Mt. Paulo anatumia historia kuwaonya Wakristo wasije wakajiamini kupita kiasi katika safari ya kiroho.

Injili: Lk 13:1-9 Yesu anatumia historia ya watu wake kuwaelezea umuhimu wa kufanya mabadiliko.
-----------------------

RUDI KWA YESU

Masomo yetu matatu yanaongelea kuhusu huruma ya Mungu katika kuwaadhibu watoto wake na kuwapa nafasi ya pili licha ya kurudia rudia kwao makosa. Ingawaje huruma ya Mungu na upendo wa Mungu daima upo juu yetu ili ufanye kazi lazima tushirikiane na neema ya Mungu. Ndio maana anatuita kipindi hichi cha Kwaresima tuweze kuungama dhambi zetu nakuanza kuzaa matunda mema, matunda ya upendo, huruma, msamaha na uaminifu. Somo la kwanza linatuonesha jinsi Mungu alivyo na huruma kwa kumchagua Musa kwenda kuwaokoa watu wake kutoka nchi ya Misri. Mungu wa Abrahamu, Yakobo na Isaka anamtokea Musa na kujitambulisha kwamba atakuwa na watu wake na anamuahidia ulinzi wake. Anaeleza kwanini anamchagua Musa, nia ni kuwakomboa watu wake na kuwaleta katika nchi ya ahadi. Anataka kurudia agano lake kama alivyofanya kwa Abrahamu kuwapa nchi ya maziwa na asali na kuwaponya magonjwa yao yote. Anawavika taji ya ukarimu na huruma.
Katika somo la pili linatuonya kwamba Mungu wetu ni mwenye huruma lakini pia ni Mungu anayeadhibu. Paulo anawaambia watu wa Korintho kwamba wanapaswa kujifunza kutoka katika historia ya wana wa Israeli jinsi walivyo adhibiwa na Mungu kwasababu ya dhambi zao, waliadhibiwa na Mungu mwenye huruma na mwenye haki. Mungu huyu mwenye huruma na mapendo anawahitaji watoke katika uasherati na kuabudu miungu mingine.

Somo la Injili linaonsha ni kwa jinsi gani Mungu huadhibu watu wake kwa kuwapa adabu na kuwaalika katika kutubu dhambi zao, kufanya maisha yao kuwa mapya na kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu. Yesu akiwakumbusha matukio mawili ya waisraeli, Yesu anawaalika watubu na kufanya maisha yao kuwa mapya. Katika mfano wa mti usio zaa matunda, anataka kuwaambia kwamba daima Mungu hawaachi mara bali huwapatia muda ili waweze kutubu kwa mara nyingine ili waweze kuzaa matunda tena. Mungu daima huwa mvumilivu na kumsubiri mdhambi aweze kutubu.
Tunapaswa kutafakari juu ya kuongoka kwetu na kufanya maisha yetu kuwa mapya. Tunapaswa kukuwa huku tukitimiza majukumu yetu katika ukomavu wa hali ya juu. Mara nyingi wengi wetu tunakuwa wakomavu katika mambo mbali mbali ya dunia lakini sio katika sala, kuhudhuria misa na kuishi Imani yetu ya Kikristo. Toba ni kitu muhimu katika maisha yetu ili kutimiza hili. Wito wa kuongoka ni kitendo kinacho jenga tena upya uhusiano wetu na Mungu. Ni kitendo kinacho unda tena upya mwanadamu kwa kuvishikiza vipande vilivyo vunjika vya maisha yetu. Yesu ndiye anayejua kutuunda tena, anajua upana wetu na urefu wetu na kututengeneza kama tulivyokuwa mwanzo.
Mara nyingi tumekuwa kama miti isiyozaa matunda. Tumecheza kwenye dhambi na hakuna neema yeyote ndani mwetu. Pamoja na hayo Mungu bado anatuvumilia na kutuhurumia akitusubiri tuweze kuacha mwenendo wetu mbaya na kumrudia. Tusidharau muda huu ambao Mungu anaotupa na kumuona Mungu ni mjinga, tujitoe na kuacha dhambi ili tuweze kuwa na Amani na Mungu na Mungu atafurahia matunda yetu.

Sala:
Bwana wa huruma, ninakuomba niweze kuhisi huruma yako na upendo wako na kufanywa kuwa mtu mpya.

Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni