Ijumaa, Machi 18, 2022
Ijumaa, Machi 18, 2022,
Juma la 2 la Kwaresima
Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28;
Zab 105:16-21;
Mt 21:33-43, 45-46
UPENDO UNAOTESEKA
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na ujumbe wa Yusufu kuuzwa Misri na ndugu zake. Ndugu zake walimuonea wivu kwa sababu ya vipaji alivyogawiwa na Mwenyezi Mungu na kutokana na upendeleo aliokuwa nao toka kwa Baba yao. Badala ya ndugu zake kushirikiana naye ili kwa pamoja wayafaidi mema ya nchi, wao waliona wivu, wakamuona kama tishio na hivyo wakaamua kumuuza Misri. Cha ajabu ni kwamba kule Misri alizidi kubarikiwa na Bwana na kufanywa Msimamizi wa mali za Pharao na mwishowe wakaja kumpigia magoti.
Hili lilimtokea Yesu pia-yeye alichukiwa na Wafarisayo kutokana na wivu tu-kwamba Yesu anapata umaarufu na wafuasi kuliko wao. Lakini mwishowe, yule waliyempiga na kumuua, walimkuta akitawala, akipigiwa kila goti na viumbe vyote mbinguni na duniani.
Sisi ndugu zangu tusitake kumchukia yeyote. Wapo wenye uwezo zaidi yetu, wapo watakaokuwa maarufu zaidi yetu. Wengine tutawaona wakizaliwa lakini watakuja kuwa maarufu zaidi yetu. Tuwapokee, tushirikiane nao. Tukiwachukia hakika hatutaweza kuzuia riziki zao au baraka zao. Ukiwachukia utawashangaa ndio wanabarikiwa zaidi-wapo watu wa namna hii-ukiwapiga teke ndio wanasogea hatua nyingi mbele. Bahati ya mtu haizibwi na mwanadamu. Tusitake kuja kuona sonu baadaye, tuachane na chuki za zisizo za msingi.
Kwenye somo la injili, Yesu anajitangaza kwamba yeye ni jiwe lililokataliwa na waashi na hakika limekuwa jiwe kuu la msingi. Yesu anaeleza kwamba Wafarisayo watajitahidi kumwandama wakifikiri kwamba ndio wamemteketeza lakini mwishowe watakuja kushangaa akiwa katika utukufu wake-yaani lile jiwe lililokataliwa na waashi-ndio litakalokuja kuwa jiwe kuu la msingi.
Hii imetokea kwa wengi, wapo waliokataliwa kwamba hawafai lakini mwishowe ndio wamekuja kuwa tegemeo kwa jamii, familia, taifa na kanisa. Tuepuke kumhukumu yeyote kutokana na kabila, taifa, rangi, historia au familia. Mungu aweza kumkweza yeyote. Tushirikiane na wenzetu ili kwa pamoja tuyafurahie mema ya nchi. Wengi tumeshindwa kuyafurahia mema ya nchi kutokana na wivu, dharau na kuwachukia wenzetu. Tupambane na vilema hivi ili tupate kufurahia mema ya nchi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni