Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Machi 06, 2022

Karibuni sana ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana kwenye Dominika yetu ya leo. Leo ni dominika ya kwanza ya kwaresma. Ni kipindi cha kuomba toba kwa sababu ya madhambi na udhaifu wetu kama wanadamu. Ni kwa sababu ulimwenguni hatuishi malaika, wapo wanadamu dhaifu kama mimi na wewe, hata kama hutaki kutenda dhambi, utasababishiwa tu. Lakini ukishatenda, basi itakuchafua na hivyo itakubidi kuungama kwani hatuwezi kumfikia Mungu katika dhambi. Na mbaya zaidi ukiiacha dhambi ikae na wewe, itakufanya mpango Mungu aliouweka juu yako ubadilike, ushindwe kutimia, dhambi ni adui mkubwa. Na kitu kinachookoa ni toba.

Ukifanya toba, unaruhusu ule mpango Mungu aliokuwekea urudiwe, upate kukamilika, wengi wetu tungatakiwa tuwe mbali lakini dhambi imeturudisha nyuma. Dhambi inakufanya unatumia muda wako vibaya. Ebu mwanafunzi ajaribu kulinganisha matokeo ya mtihani alioufanya akiwa anaangalia picha mbaya katika simu na matokeo ya ule alioufanya akiwa katika sala. Utashangaa, matokeo yatakuwa tofauti. Dhambi inatufanya tupoteze pia rasilimali-na hivyo unajikuta ukirudi nyuma hatua kumi-ebu fikiria jinsi kuhonga wanawake kunavyotufanya maskini? Watu hawajengi kutokana na uzinzi, kuhonga tu kila siku. Au angalia jinsi ulevi unavyorudisha watu nyuma? Hivi vyote sio vitu vizuri, yabidi tupambane navyo.

Kipindi hiki cha kwaresma tunakumbushwa ubaya wa yote hayo na tunaambiwa sasa kwamba ni lazima kumrudia Bwana-kwani dhambi zinatuangusha, na hii kumrudia lazima kuwe endelevu, sio tu kwa siku moja au kipindi kimoja tu katika mwaka. Huu ndio ujumbe mkuu wa kwaresma ndugu zangu.

Sasa, kwenye somo letu la kwanza leo, tafakari ya neno la Bwana linatueleza kwamba Bwana Mungu wetu lazima aabudiwe, apewe kipaumbele maishani. Hii ndiyo hatua ya kwanza. kwenye somo la kwanza, Musa anawaeleza hawa wana wa Israeli kwamba hakika wasimsahau Mungu pale watakapoingia katika nchi ya ahadi. Katika wafanyalo, wakumbuke historia yao, kwamba wao walikuwa watu wa utumwani, lakini wakaokolewa na Bwana. Hivyo watambue hili na huu ulikuwa ndio msingi mkubwa wa hekima. Hivyo leo anawaeleza kwamba utakapoingia nchi ya ahadi (kipindi hiki wana wa Israeli walikuwa jangwani wakitangatanga-walikuwa wakilishwa na mana toka mbinguni), utakuwa hauli tena mana, mtakuwa mnakula mazao ya nchi ya kawaida. Lakini hata hayo ukumbuke kwamba ni mimi ninakulisha, ninayeyawezesha yote.

Hivyo, mazao ya kwanza yalete kwa kuhani kama malimbuko na kuhani akuelezee namna jinsi nyie mlivyokuwa wewe na Baba zako kule jangwani na leo umewezeshwa kupata mazao-lazima ubakie kujua kwamba ni Mungu anayekulisha bado. Hili lilipaswa lisifutike kichwani mwao. Hili ni lazima litendeke ili Israeli itambue kwamba mwanadamu haishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Bwana, pia, ni lazima jambo la namna hii lilipaswa kutendwa na wana wa Israeli ili kuonesha kwamba ni Mungu tu wa kuabudiwa na si nguvu nyingine katika ulimwengu huu.

Pia hili lilipaswa kutendeka ili kuepuka kishawishi cha Israeli kumwacha Mungu na kugeukia nguvu nyingine.
Hivi ndivyo vishawishi vikuu ambavyo mwanadamu hapa ulimwenguni anapambana navyo-na tunapaswa kuvishinda.

Yesu alipambana navyo pia. Katika injili, kishawishi cha kwanza ni kile cha chakula-Yesu anaambiwa ageuze mawe yawe mkate; yaani ni kama mwanadamu anayeambiwa ati kwamba jitegemee mwenyewe bila Mungu. Yesu anajua kwamba kule jangwani japokuwa kulikuwa na ukame, wana wa Israeli waliweza kulishwa kwa mana na maji ya mwambani. Hii mana ilitokea kwa nguvu ya neno la Bwana. Waliokazana kujilisha chakula chao wenyewe na kutaka kurudi misri, waliishia kufa njiani, walishindwa. Yesu anamueleza kwamba siwezi kutegemea nguvu zangu mwenyewe kwani mwanadamu hatushibishwi kwa njia ya mkate tu bali kwa neno litokalo katika kinywa cha Mwenyezi Mungu. Huu ni kukiri ukuu wa mwenyezi Mungu.

Kishawishi cha pili ni cha kuonyeshwa milki za ulimwengu ilia apate kuzitawala kama atamwabudia Ibilisi. Hiki ni kishawishi cha kutaka kumpindua Mungu, kutumia uwezo wako kumyanganya Mungu madaraka, Yesu alikuwa amekwishakabidhiwa mamlaka yote mbinguni na duniani. Lakini ilibidi tu asubiri tu muda ili baada ya kifo yote hayo ayapokee. Lakini shetani anakuja kama haraka anamwambia yachukue haraka. Yesu anamjibu kwamba siwezi kumpindua Mungu maishani. Imeandikwa kwamba ni lazima nimtegemee yeye kila wakati.

Kishawishi cha tatu ni kuambiwa ajitupe ili basi malaika wa Mungu wamlinde. Hapa ilikuwa ni kumjaribu Mungu, kujua kwamba umepewa mamlaka na unalindwa lakini unaanza kucheza na ile nafasi. Ni kama mtoto aliyeshika wembe kwa mara ya kwanza anaanza kukata nao kila kitu. Au padre aliyepata upadre na kuanza kutumia yale madaraka yake vibaya. Au umeambiwa hii saa ni water resistant na wewe unaanza kuidumbukiza kwenye maji kila siku au kuihifadhi kwenye maji. Huku ni kujaribu. Na ukishakua na kitu fulani na ukianza kukichezea chezea kila siku kinaishia kuharibika haraka haraka tu.

Hivi ndivyo vishawishi vilimkabili Yesu, na vinamkabilia pia mwanadamu hadi siku ya leo na tunaalikwa kupambana navyo huku maishani.

Yesu aliweza kuvishinda kwa sababu aliyajua maandiko matakatifu. Biblia kama huijui inaweza ikatumiwa vibaya kukuangusha, kuhalalisha hata uasherati na nyumba ndogo. Shetani anatumia baadhi ya mistari kukuangusha. Nawe pia jiandae kupambana naye kisawasawa. Ijue Biblia umshinde shetani. Kama huijui, atakuwa anaitumia kila siku kukukamata.

Lakini ukishaijua, atakuwa anakukimbia tu. Hivyo tusome Biblia jamani na ndio maana mimi katika mahubiri au mafungo yangu au chochote nifanyacho lazima nianze na Biblia tu.

Kishawishi cha kutaka kujilisha ndicho cha kwanza kinachotuangusha kila siku. Huwa tunakazana sisi wenyewe kugeuza mawe yawe mkate kila siku. Hatutegemei nguvu za Mungu, tukiamka hatusali na kumweleza Mungu atupe mkate wetu wa kila siku. Unakuta mtu aakwenda kuuza vitumbua vyake apate riziki lakini hamwombi Mungu abariki kazi yake hii ya kuuza vitumbua.

Unataka ugeuze mawe yawe mkate kwa nguvu zako. Na nakueleza kwamba hutakaa ushibe ndugu yangu. Jikabidhi kwa Bwana ukijua kwamba unalishwa na kushiba kwa neno litokalo kinywani mwake.

Kishawishi namba mbili cha kuacha kumsujudia Mungu, kinatukumba na sisi kila siku. Tunaabudu kazi, akili, na watu maarufu. Tunaabudu pia biashara zetu. na kumuacha Mungu. Hiki ndicho kishawishi kinachoukumba ulimwengu. Mungu ndiye wa kuabudiwa, vishawishi vya namna hii vipatie maelezo:kwamba imeandikwa tumtumainie Mungu peke yake, na wala si mwingine. Hivyo tuepuke kuabudu simu zetu, fedha, marafiki, au watu maarufu.

Kishawishi cha tatu cha kujaribu nguvu za Mungu. Hiki pia kinatokea. Ni kama mtu anayetaka kujaribu kisu kama kinakata. Epuka kumtumia Mungu namna hii. Yesu hakutaka kumfanyia Mungu maigizo, ajitupe halafu adakwe kama maonesho ya sarakasi. Hii ni kumjaribu Mungu. Nguvu na uwezo wa Mungu utumike kwa imani na sio kama mazingaumbwe. Ndivyo ilivyo na kwetu pia. Kama umepewa uwezo au nafasi, usiitumie kimaigizo. Itumie serious, usicheze na uwezo. Ni kama padre anayechezea uwezo wake aliyepewa na Mungu, usiuchezee hata kidogo.

Hivi ndivyo vishawishi vitukumbavyo, vinatuondoa karibu na Mungu. Lazima tupambane navyo. Mwabudu Mungu siku zote.

Maoni


Ingia utoe maoni