Jumatatu, Machi 07, 2022
Jumatatu, Marchi 7, 2022.
Juma la 1 la Kwaresima
Law 19: 1-2, 11-18;
Zab 19: 8-10, 15;
Mt 25: 31- 46
NI NANI NDUGU YANGU ALIYE MDOGO?
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka katika kitabu cha Walawi ambapo tunamkuta Mungu akiwakumbusha wana wa Israeli kwamba Mungu wao ni mtakatifu na hivyo wajitahidi ili wahakikishe kwamba na wao wanakuwa watakatifu. Ni kwa namna hii tu ndio watakapoweza kuungana na Mungu na kumfikia kama wanadamu na taifa teule la Bwana Mungu wetu.
Hivyo, Mwenyezi Mungu anawaeleza kwamba lazima wazishike amri-amri zitakazowafanya kuwa watakatifu. Amri hizi zinasisitiza juu ya kumpa Mungu nafasi ya kwanza kuliko vitu vyote-kuepuka kuabudu miungu mingine. Hilo ndilo linalosisitiziwa. Halafu, zinatuambia pia tuwaheshimu binadamu wenzetu tunaoishi nao hapa duniani. Tuwaone kama viumbe viteule vya Mungu na hivyo tusiwaonea bali tuwaheshimu na kuwapatia heshima zao. Namna hii tutaweza kuwa watakatifu na kwa huu ndio wito tulioitiwa na Mungu ndugu zangu.
Hivyo, duniani hatuwezi kuishi kirahisi kirahisi tu. Lazima tuwe na majukumu ya kutekeleza, lazima tujitoe sadaka ili kumpendeza Mungu na wenzetu wapate kuishi. Mara nyingi wanaoharibu ni wale wanaopendelea mambo yawe kirahisi rahisi tu, tusibanwe banwe sana, mambo yaende tu, nifanye mambo yangu. Watu wengi wanataka hivyo na watu wa namna hii huwa wabinafsi na hawa ndio wanaoiletea dunia matatizo.
Ndugu zangu, unapokiuka na kukataa kuishi amri ya Bwana, unamuumiza mwenzako na Mungu pia. Hili tumelisikia katika injili ya leo. Unamfanya mwenzako akose chakula, afungwe gerezani kwa dhuluma, akose hata nguo ya kuvaa na wagonjwa wafe kwa kukosa dawa. Mfano. Angalia rushwa zinavyowafanya watu wasisome, au uzembe wangu daktari umewaua wangapi au mimi hakimu mla rushwa nimewafunga wangapi bila hatia au mimi mzazi nisiyetimiza wajibu wangu nimewafanya watoto wangu na mke wangu wateseke namna gani. Yote haya ni kukosa kutimiza amri ya Mungu.
Na katika injili yetu atatuhukumu kwa kututupa katika tanuru ya moto kwani matendo yetu yamewaumiza wengi na wenzetu wanapoumia wanamlilia na wakimlilia Mungu anajibu kama tulivyosikia katika injili.
Hivyo, ndugu zangu, kabla ya kufanya tendo lolote tuchunguze hasara zake kwetu na kwa wenzetu. Kama unataka kupokea rushwa jaribu kuangalia ni watu wangapi wanateseka kutokana na wewe kufanya hivyo, kama ni hakimu mla rushwa au daktari mzembe au mzazi mzembe, askari mla rushwa, dereva asiyejali-angalia ni watu wangapi wanaumia kutokana na uzembe wako. Angalia laana inayokuelekea kutokana na kilio cha hao watu, kutokana na uzembe wako, angalia pia kilio cha watoto wao watakapokuwa wanakulaani. Tumuombe Mungu tutafute utakatifu zaidi ili tupate kustahilishwa kumuona Mtakatifu mwenyewe.
Maoni
Ingia utoe maoni