Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Machi 09, 2022

Jumatano, Marchi 9, 2022.
Juma la 1 la Kwaresima

Yon 3:1-10;
Zab 51:3-4,12-13,18-19;
Lk 11:29-32

KUMKUBALI YESU NA UPENDO WAKE!

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza leo tunakutana na Malkia Ester akilia mbele za Mwenyezi Mungu. Yeye analia kwa sababu ya Wayahudi wenzake waliokuwa wakiteswa na baadhi ya viongozi katika ufalme wa wapersia. Ester alikuwa akifurahia maisha mazuri yasiyotindikiwa katika Ikulu ya Mfalme wa Persia kama Malkia. Lakini pembeni, Wayahudi walikuwa wakichukiwa na kuuawa.
Kila mara alisikitika kukutana na miili ya Wayahudi waliouawa na kutelekezwa njiani. Walijitokeza viongozi waliokuwa na chuki dhidi ya Wayahudi na kuwachukia Wayahudi kwa kiasi kikubwa. Ester hakuridhika kuona hili. Aliamua kunyanyuka kuwatetea watu wake. Aliomba mbele ya Mwenyezi Mungu aweze kutimiza kazi yake ya kuwafanya ndugu zake wasitupwe katika mateso.
Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kusali sala kama ya Ester. Ni kipindi cha kushuka na kutoka katika Ikulu zetu, kutoka katika anasa zetu na kuja kuona maumivu ya wenzetu waliopo chini, maumivu ya wanaonyanyaswa na umaskini, magonjwa, chuki za moyoni, uadui na ushirikina.
Wengi tumetawaliwa na ubinafsi. Wapo tuliofanikiwa lakini hatuwaangalii ndugu zetu. Hakika tunawahitaji watu wenye roho nzuri kama kina Ester. Tuachane na ubinafsi wetu na kuangalia wazazi wetu wanaonyanyaswa na umaskini na ugonjwa, na kuwatazama watoto wa ndugu waliotelekezwa, wanaokosa ada ya shule au chakula cha kila siku. Tujifunze kuwa kama Ester. Kina mama wengi leo tuombe kuwa kama Ester hasa kwa watoto, ndugu na waume zetu. Tuwaombee kwa moyo mnyenyekevu. Tuachane na kuwasengenya kwa umbea.
Katika somo la Injili, Bwana Yesu anatambua umuhimu wa mwanadamu kupeleka maombi yake kwa Mwenyezi Mungu. Anasema kabisa kwamba tuombe na hakika tutapewa. Ili tuweze kupata lazima tuombe. Na katika kuomba, hakuna kikomo kwani ni juu ya yule anayeombwa kupanga muda na wakati wa kujibu maombi. Na yeye hutoa kwa kadiri ya sisi tutakavyosaidika.
Mara nyingi Mungu hatoi vitu ambavyo havitatusaidii kwa wakati uliopangwa na muafaka. Hivyo tujifunze kushukuru hata pale tuombapo na kufikiri kwamba hatujapokea tulichokiomba. Mara nyingi mawazo ya Mungu sio mawazo yetu. Kwa kitendo chake cha kutunyima kile tuombacho sasa, baadaye tutaweza kuja kutambua faida ya sisi kunyimwa kile tulichoomba. Tujifunze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila jambo na tuombe ili matakwa yake yatimizwe.

Maoni


Ingia utoe maoni