Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Machi 10, 2022

Alhamisi, Machi,10, 2022.
Juma la 1 la Kwaresima

Est C:12, 14-16, 23-25;
Zab 138:1-3, 7-8
Mt: 7:7-12


OMBENI NANYI MTAPEWA!


Ndugu zangu wapendwa karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu Asubuhi ya leo. Tukianza na wimbo wetu wa katikati unaosema siku ile niliokuita uliniitikia ukanitia nguvu na kunifariji nafsi. Mzuburi anamshukuru Mungu kwani alipokuwa katika taabu alimwita Bwana naye akawa ndio chanzo cha nguvu na faraja zake.

Wimbo huu unatilia mkazo somo la kwanza kwani wakati Waisraeli walivyokuwa katika hatari ya kuangamizwa na Hamani, malkia Esta alifunga na kusali na kweli Mungu akawafariji waisraeli nafsi kwa kuwaokoa na mkono wa Hamani na akawapa nguvu. Tukimuomba Bwana vizuri tunapokuwa katika matatizo daima anatusaidia. Hata kama tunapitia katika magumu ya namna gani yeye atatusikia kama tutamuita vizuri na kwa moyo.

Somo la Injili linatilia mkazo tena kwamba wakutusaidia kutua mizigo yetu tunapoelemewa ni Yesu. Sisi tumuite kwa Unyoofu kama Malkia Esta alivyomuita Mungu kwa unyoofu. Hakika Mungu hatatuacha. Yeye daima tukimuita vizuri atatusikia. Mara nyingi pengine Mungu hatusikii kwasababu tunaomba ili Mungu awalipe visasi wale waliotukosea. Tunatamani kama Mungu angewaangamiza na kuwaulia mbali. Hatuombi Mungu awabadilishe na kuwafanya wema, ila sisi tunaomba atue mizigo yetu kwa kuwateketeza maadui wetu na kuwafutilia mbali kabisa.

Tumuombe Mungu atusaidie tukimbilie kwake kutuoa mizigo yetu. Tusikimbilie kwa viumbe wake aliowaumba. Yeye ananguvu na mizigo yetu ataitua hakika. Sisi tunamkimbilia mganga, tukidhani yeye ndio atatutia nguvu na kutifariji. Ukweli ni kwamba Bwana ndiye mfariji wetu tumkimbilie yeye Kama Esta alivyofanya akabarikiwa na Waisraeli wote.

Maoni


Ingia utoe maoni