Ijumaa, Machi 11, 2022
Ijumaa, Marchi 11, 2022,
Juma la 1 la Kwaresima
Eze 18:21-28;
Zab 130: 1-8;
Mt 5:20-26.
KUWA MWEMA!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, Bwana Yesu anazungumzia juu ya haki inayopaswa kuizidi ya waandishi na mafarisayo: hawa walikuwa waalimu maarufu enzi za Yesu na waliheshimika kama watakatifu na mfano wa kuigwa. Lakini Yesu anasisitiza leo kwamba kama wafuasi wake hawatajitahidi ili kuwa na msimamo mpana zaidi kuliko viongozi hawa-kwa hakika hawataweza kuingia katika ufalme wa Mungu.
Hii ni kwa sababu mafundisho na mitazamo ya viongozi hawa ilikuwa na upungufu mkubwa. Mafundisho na misimamo yao ilikuwa imejikita katika matendo ya nje nje ya kujionesha. Walishindwa kuoanisha nia safi na matendo yao. Na watu walikuwa wakiwaiga watu wa namna hii. Yesu anasisitiza kwamba wema lazima uanzie moyoni kwanza. Lazima mawazo ya mioyo yetu yaoanishwe na matendo yetu kwani Mwenyezi Mungu hutazama moyo wa mtu. Hivyo tukazane kugeuza mawazo ya mioyo yetu yahakikishe kwamba yanafanana na kile tunachokitenda nje.
Kipindi hiki cha Kwaresima twaweza kujikuta tunatoa misaada mingi kwa watoto yatima, na wasiojiweza lakini matendo haya pia yaendane na mioyo yetu. Kila tunapofanya tendo la huruma, mioyo yetu igeuzwe, ipate kuwa mipole zaidi, na iwe ya huruma zaidi-na sio kuwa na kiburi au majivuno na kujitangaza. Pia tuepuke kuweka vinyongo juu ya wenzetu, au kuwawazia yaliyo mabaya. Pale ilipo sadaka yetu, uwepo pia na moyo wetu.
Nabii Ezekiel katika somo la kwanza Nabii Ezekiel anazungumzia juu ya ukweli kwamba dhambi huua. Dhambi kwa uhakika ni mbaya na anayeiendekeza, huishia katika kifo na dhambi inayotendwa sasa ndio hatari zaidi. Nabii anatangaza kwamba kama tuliwahi kutenda matendo mazuri na makuu zamani hayapaswi kutumika kwenye kujitetea hasa pale tunapotenda uovu kwa sasa. Ya zamani yameshapita; muhimu ni ya sasa. Basi tujifunze kwamba wakristo ni watu tunaopaswa kuboresha maisha yetu kila kukicha. Kila kukicha tunuie kutenda matendo mazuri; wema wetu unapaswa kukua kila siku na sio kurudi nyuma na kukumbukia ya zamani. Ya zamani hayatatuokoa hata kidogo.
Maoni
Ingia utoe maoni