Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Machi 13, 2022

Jumapili, Machi 13, 2022.

Dominika ya 2 ya Kwaresima

Mwa 15:15-12.17-18;
Zab 27:1.7-9.13-14;
Flp 1:8-10;
Lk 9:28b-36.

KWARESIMA: MUDA WA KUMFAHAMU YESU!

Juma la kwanza la Kwaresima linatuandaa, kufanya matendo ya kwaresima, kusali, kufunga na kutoa sadaka. Inakuwa ni hatua kwetu kutengeneza hali nzuri ya kuingia katika kipindi hichi kwa undani. Jumapili iliopita ilituandaa kuhusu majaribu, na umuhimu wa kusafisha dhambi zetu rohoni mwetu. Yesu alituanyesha njia ya kumshinda shetani na dunia na pia vishawishi vya miili yetu, alipokuwa jangwani. Leo anajifunua kwa njia ya Kugeuka sura kutualika wote kwenye utukufu alio nao na Baba yake. Kwa njia ya kungara sura tunaalikwa kwenye ufufuko wa miili, wakati tutakapo kuwa huru kuhusu dhambi. Kama mwili wa Yesu ulivyokuwa katika utukufu, ndivyo miili ya watakatifu itangaa. “Utukufu ulionipa mimi nimewapa wao” (Yn 17:22).

Uhusiano unakuwa kadiri ya muda. Tunawafahamu watu zaidi kadiri ya muda unavyo sogea. Mitume pia lazima na wao waliendelea kumfahamu Yesu kadiri ya muda ulivyokuwa ukisogea. Uhusiano wao ulianza alivyo waita hapo awali. Waliishi naye na kumsikiliza na kushuhudia miujiza na uponyaji mbali mbali. Uelewa wao lazima utakuwa ulikuwa kadiri ya muda, mpaka Petro akafikia kiwango cha kusema “Wewe ni Masiha Mwana wa Mungu aliye hai”. Lakini Petro alimpinga alivyosikia habari ya kifo chake, na Yesu alitambua kuwa Wafuasi wake hawajamfahamu vizuri bado. Walimwelewa vibaya kuwa kama Masiha wa kidunia atakaye iongoza dunia daima. Ndio, maana baada ya siku sita hivi Yesu awaliwachagua Petro, Yohane na Yakobo kwenda mlima na kushuhudia kungara kwake kwa sura inayoelezewa leo katika Injili.

Kungara sura kwa Yesu kunatokea wakiwa juu ya milima. Mlimani palijulikna kama sehemu ya kukutana na Mungu. Wakati Yesu anageuka sura mavazi yake yalingaa sana na uso wake ulingara. Taswira hii alioionyesha Yesu ni hali ya utukufu ambayo itakuja baada ya maisha ya ulimwengu huu. Musa na Elia ambao katika tamaduni ya Wayahudi waliwakilisha mambo mawili muhimu ya Wayahudi. Sheria na Manabii. Musa na Elia walikuwa ni watu ambao walipata kuwasiliana na Mungu wakiwa katika milima. Na waliwaongoza watu wa Israeli kumrudia Mungu.

Kwa kuangalia hali hii ya kugusa na kuogopesha, Petro anaomba kujengwe vibanda vitatu kimoja cha Yesu, kimoja cha Elia na kimoja cha Musa. Petro alipenda hii hali iendelee kuwapo. Mungu anaingia kati na kumfunua mwanae (Mwana wa Mungu) kwa wafuasi “Huyu ndiye Mwanangu mpendwa…” Mitume wanaogopa na wanainamisha nyuso zao. Walivyo nyanyuka walikuta kila kitu kikiwa katika hali yakawaida. Tukio hili ni lazima lilikuwa ni la nguvu sana kuliko tukio lolote lile ambalo mitume hawa watatu waliweza kulishuhudia. Katika tukio hili la kungara sura, Umungu wa Yesu ulifunuliwa kwao. Waliweza kufahamu Yesu ni nani na kwanini Yesu alikuwa akiongelea kuhusu kifo na ufufuko . wafuasi waliweza kuja kumfahamu Yesu vizuri zaidi wakati wa Karamu ya mwisho, mateso yake alivyokuwa pale Getsemane, mateso yake, kifo na kufufuka. Muda wote waliokuwa na Yesu waliweza kuja kumfahamu Yesu na kutambua nini maana ya kuwa wafuasi. Nasi ni hivyo hivyo.
Katika somo la kwanza tunasikia kuhusu kuitwa kwa Abrahamu. Abrahamu anajibu wito wa kwanza kabisa wa Mungu. Na ni baada ya muda tu alikuja kumfahamu Mungu vizuri na utume wake kwa ajili yake. Hivyo, tunavyopata muda wa kuwa na Mungu zaidi ndivyo tunavyozidi kuendelea kumfahamu zaidi, na kadiri tunayo endelea kumfahamu Mungu, ndivyo tunavyo fahamu mpango wake kwetu.
Kwaresima ni kipindi cha kutafakari na kukaribisha neema ya Mungu katika maisha yetu. Sio muda tu wakuachia vitu, bali pia ni muda wakupokea zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Mungu hajatusahau sisi watoto wake ila ni sisi tuliomsahau yeye na kukimbia uso wake. Leo, upendo unafunuliwa kwetu kwa njia ya Yesu. Yesu kwa njia ya ufufuko anatufanya sisi kuwa sehemu ya mpango wa Mungu tangu milele, kuwa watakatifu na kupendwa na Mungu kwa kuwa daima mbele zake. Ufufuko unaleta kwetu mwanga katika maisha yetu kama wa kungara sura kwa Yesu, kiasi kwamba hakuna giza linalo baki.

Maandiko matakatifu yanatuonesha njia ya kwenda katika muelekeo huu. Kwanza kabisa, kuwa na muda wa kusali kama Yesu. Pili ni kumfahamu Yesu, na hili linafanyika kwa kutafakari Maandiko Matakatifu, Mungu aliwaambia wafuasi kwamba “Msikilizeni yeye” pia Neno la Mungu linafunua nafsi ya Yesu kwetu sisi kila siku. Tatu, tuwe tumeungana katika jumuiya zetu. Kama mitume watatu walivyo pata kumshuhudia Yesu, na kushiriki katika mwanga uliofunuliwa na Mungu. Hili linawezekana daima tunavyo shiriki katika Ekaristi Takatifu, tunaitwa wote kuunganika katika kungara kwa Yesu katika Ekaristi takatifu. Na mwisho kabisa, kushiriki katika mahusiano mazuri na wenzetu. Mitume hawakuweza kushirikisha walio yaona muda ule, bali walishirikisha baada ya ufufuko wakati wamesha elewa maana kamili ya kungara kwake sura, walishirikisha wengine kwa kuhubiri habari Njema. Sisi pia tunaitwa kutangaza kungara kwa sura kwa Yesu kwa kuwatangazia wale wote waliotengwa. Tunaitwa kutambua matendo ya roho na matendo ya nje ya huruma: kuwalisha maskini, kuwapa maji walio na kiu, kuwavisha wasio na nguo, kuwakaribisha wasio na makao, kuwaponya wagonjwa, kutembelea wafungwa, kuwazika wafu, , kuwasaidia walio na mashaka, kuwaelekeza walio wajinga, kuwa elekeza wadhambi warudi, kuwafariji wenye matatizo, kuwasamehe walio tukosea, kuchukuliana kwa huruma wale wote wanao tuumiza na kuwaombea walio wazima na wafu.

Sala:
Bwana, ninaomba nifarijike kwa utukufu wako na ukweli wako. Ninaomba nikumbuke utukufu huu ninapo tembea katika changamoto mbali mbali katika maisha. Utatembea mbele yangu na kunitangulia nikikuamini wewe. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni