Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Machi 17, 2022

Alhamisi, Machi 17, 2022.
Juma la 2 la Kwaresima

Yer 17:5-10;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 16:19-31

UPENDO WA MUNGU KWA MASKINI

Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari ya neno la Bwana inatusisitizia juu ya kumtumainia Mungu. Somo la kwanza linaanza kwa ushuhuda wa nabii Yeremia. Jana tulisikia akimlilia Mungu amuepushe na mkono wa adui katili aliyetafuta maisha yake ili amteketeze. Yeye alisalitiwa na kila mtu na hivyo ilibidi amtumainie Mungu tu. Mungu alizidi kumuokoa na leo sasa anawatangazia watu juu ya faida iliyo katika kumtumainia Mungu, anasema ni kama kuotesha mmea kando ya mto ambapo siku zote unapata maji. Yeye mwenyewe alionja kutunzwa na Bwana kama mmea uliooteshwa kando ya mto. Na sasa anawataka wenzake wamtumainie Mungu pia.
Somo la Injili tena tunakuta mwendelezo wa habari za waliomtegemea Bwana na kufanikiwa. Hawa ni akina Abrahamu na yule maskini Lazaro. Yeye hakuwa na chakula bali aliishi kwa umaskini akiokota chini ya meza ya tajiri. Yeye alitumia wakati aliokuwa nao katika umaskini wake kumshukuru Mungu kwa kile alichoweza kumpatia kilichoanguka mezani kwa huyo tajiri, alimshukuru Mungu licha ya kwamba tajiri hakumjali bali aliruhusu hata mbwa wake kulamba vidonda vya Lazaro. Mwishowe Lazaro anakufa akimshukuru Mungu kwa uhai alioweza kumjalia na Bwana alimchukua hadi mbinguni. Yule tajiri alikuwa anajivunaga, akijiona kuwa na kila kitu na kukazana kutumia nguvu zake lakini mwishowe zimempeleka motoni. Aliyetumia nguvu zake zimeishia kumpeleka motoni. Aliyemtegemea Bwana ameishia mbinguni na hivyo kubarikiwa.
Hapa twajifunza jambo muhimu ndugu zangu. Ule umaskini wa Lazaro kwa hapa duniani ulionekana kama adhabu na laana lakini kumbe ulikuwa ni Baraka. Utajiri wa tajiri ulionekana kama Baraka na ngekewa kumbe ni laana kwake. Somo hili litufunze kitu sisi tusioridhika, tunaotafuta utajiri. Waweza kujiona kuwa ni fukara lakini huo ufukara lazima kuwa tayari kujifunza Baraka iliyondani ya huo ufukara. Sisi tuliopata uwezo tujifunze kutambua hasara iliyo katika huo uwezo. Sisi wenye akili darasani au maarifa tujifunze kutambua hasara au hatari iliyo ndani ya huo uwezo au akili. Hili ni la muhimu sana ndugu zangu. Tusitamani vitu vingine vya ziada. Baraka ipo ndani ya kile Mungu alichonipa. Niache tamaa au kutafuta kuwa kama mwingine, mwishowe usije ukadhulumu watu na kuishia kuwa na mali ya dhuluma, hii inapo ingia katika maisha yetu, tutatumia hata kalamu kupindisha mahesabu ili tupate fedha za dhuluma, kumbuka Mungu anahitaji sadaka kamili ghalani mwake, hata hivyo tusijisifu kwa kusaidia maskini au kutoa sadaka kwa fedha za dhuluma. Toa sadaka kamili na saidia kwa sadaka kamili isio na mawaa. Niwe mwaminifu kwa kile nilichojaliwa. Tumsifu Yesu Kristo!

Maoni


Ingia utoe maoni