Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 22, 2022

Jumanne, Februari 22, 2022,
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa


SIKUKUU YA UKULU WA MT. PETRO (MTUME)

1 Pt 5: 1-4;
Zab 23: 1-6;
Mt 16: 13-19.


MAMLAKA YA KUTUMIKIA.

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya ukulu wa Mt. Petro. Hili ni adhimisho la cheo alichopewa huyu mtume na alikipewa na Bwana mwenyewe mara tu baada ya kumkiri kwamba yeye ni Masiha Mwana wa Mungu ajaye ulimwenguni. Yesu aliamua kumchagua mmoja kati ya wale mitume, awe halifa wake kwa dunia hii. Yeye alipokea cheo na alivuviwa Roho Mtakatifu toka kwa Yesu. Hiki ni cheo kikubwa sana. Cheo hiki ni ishara ya upendo toka kwa Yesu na sasa kiko mikononi mwa Baba mtakatifu wetu. Na hivyo yapaswa tukiheshimu cheo hiki.
Tafakari ya neno la Bwana katika sikukuu hii linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza toka waraka wa mtume Petro kwa watu wote. Hapa tunamkuta Petro akiwasihi wazee wenzake, mitume, na maaskofu wa makanisa mbalimbali wawe waaminifu na walichunge lile kundi la Mungu walilokabidhiwa na walichunge vyema.
Lengo ni hilo kundi lifike kule Yesu alikoliitia. Petro alichukua jukumu hili la kuwaambia wazee wenzake kwa sababu yeye alijua kwamba yeye alikuwa amechaguliwa kuwa kiongozi wa lile kundi na hivyo ilikuwa ni jukumu lake kuangalia kwamba lile kundi linafikia kule lilikotakiwa. Alijua kwamba uchu wa madaraka na uzembe wa viongozi ungeliangusha lile kundi zima na hivyo ilimbidi alitilie maanani hili.
Katika injili, tunakutana na Petro akimkiri Yesu kuwa Masiha. Wanafunzi wenzake hawakuwa na ujasiri wa kumkiri Yesu kama Masiha lakini Petro aliweza. Na Yesu anamwambia Petro kwamba ni Mungu mwenyewe ndiye aliyemwezesha, aliyemvuvia Roho ya kuweza kumkiri kama Masiha miongoni mwa wanafunzi wake na kwa sababu hiyo, Yesu anamwahidia makubwa, anamtakia heri na atakuwa Baba kiongozi wa mitume wote kama tunavyosikia katika somo la kwanza na yeye atawashauri sana.
Ndugu zangu, katika sikukuu hii, tunayo mengi ya kujifunza kama yafuatayo: kwanza, ni umuhimu wa cheo cha Baba mtakatifu hapa duniani. Nafasi ya Petro sasa iko katika kiti cha Baba mtakatifu. Yeye ni halifa wa Kristo na hivyo yafaa aheshimiwe na kusikilizwa. Tusikilize mafundisho yake na nasaha zake anazotoa kila siku au kila wakati wa matukio makuu makuu. Tusidharau kiti cha Baba mtakatifu. Sio kiti cha kutunga bali ni Yesu mwenyewe alikiweka.
Halafu, kila mmoja lazima akubali kuwa mwaminifu popote alipo ili awapatie mwongozo safi wakristo wenzake wanaomtumainia hasa wale walio wadogo. Usimkwaze mtu ndugu yangu. Tuogope hili. Petro anatusisitizia hili katika somo la kwanza.
Halafu, unapokuwa tayari kusema ukweli juu ya mtu fulani, bila wivu au unafiki, Mungu atakubariki tu. Yawezekana kwamba wale wanafunzi wenzake na Petro waliona kwamba kumwambia Yesu kwamba ni Masiha basi itakuwa labda wanamkweza mno na ndio maana walikaa kimya. Lakini yule aliyekuwa mkweli na mjasiri wa kusema ukweli hakika alibarikiwa.
Nasi tuwe wajasiri namna hii ndugu zangu.
Tuwasheshimu viongozi wetu wa dini. Na sisi viongozi wa dini tujitahidi kuwa mfano kwa lile kundi. Tuache matendo yanayowakwaza wenzetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni