Jumatatu, Februari 21, 2022
Jumatatu, Februari 21, 2022.
Juma la 7 la mwaka wa Kanisa
Mk 9: 14-29.
NGUVU YA AJABU YA IMANI!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati inasisitiza juu ya ukuu wa sheria ya Bwana kwamba sheria hii inayo uwezo wa kuburudisha moyo. Sheria hii hujidhihirisha katika adabu faraja, haki, upendo na furaha. Haina lengo la kulipa kisasi au kujipatia faida binafsi. Lengo lake ni kuleta amani na uhai kwa wote.
Zaburi hii imetumika kwenye kusisitiza ujumbe wa somo la kwanza ambapo Mt. Yakobo anafundisha kuhusu tofauti ya hekima ya kibinadamu na hekima ya Kimungu. Anasema kwamba hekima ya Kimungu haina tamaa, inapenda amani na haki, imejaa huruma na imejikita katika kutenda wema.
Sisi tutumie ujumbe huu wa Mt. yakobo kuchunguza juu ya nyendo zetu ili zipate kutulia katika hekima ya kimungu. Kuna wakati tunangangania kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ili tupate sifa za haraka haraka. Lakini mara nyingi hii yaweza kuwa kinyume cha hekima ya kimungu kwani ni dalili za tamaa. Upo pia wakati tumefika mbele ya Mungu na mlolongo mwingi wa maombi au tunakwenda kuomba kwa wenzetu tukiwa na mlolongo mwingi wa maombi. Hapa ni dalili za tamaa na kutokutosheka na kile kidogo kilichopo. Hekima ya kimungu itufundishe kwanza kuridhika na kidogo, na katika kuomba tuombe kihatua hatua. Hekima ya kimungu inatufundisha kuwa na kiasi katika kila eneo. Hata kama ni katika kuongea, kula, kuomba, kusali au kufanya mambo yoyote lazima pawepo na kiasi. Tuombe kuwa watu wa kiasi.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anamponya mgonjwa aliyeshindikana kuponywa na baadhi ya wanafunzi wake. Hakika kitendo cha wanafunzi wa Yesu kushindwa kumponya mgonjwa huyu kiliwaletea aibu kwani wengi walihoji mamlaka na uwezo wao. Yesu anamponya mgonjwa huyu. Tukio hili lilikuwa fundisho kwa mitume wa Yesu kwamba katika kuitenda kazi ya Bwana, ni roho anaye tenda. Hivyo wahakikishe kwamba siku zote wapo na Roho wa Bwana.
Wawe watu wa kusali na kufunga. Uwezo wa uponyaji hautakuja kama ushirikina ulivyo. Watakapokosa roho wa Bwana, na uwezo huo utawatoka. Hili ni himizo na fundisho kwetu kwamba maisha yetu ya ufuasi lazima yakolezwe na sala na kufunga. Hizi ni nyenzo muhimu. Hakuna sehemu yote katika Biblia ambapo Mwanadamu alimlilia Mwenyezi Mungu kwa sala na kufunga asisikilizwe. Sisi tusikuchoke kusali na kufunga. Tufunge anasa mbalimbali kama wafuasi wa Bwana, tufunge kuongea mambo machafu, tufunge kula au kununua kila tunachokutana nacho mbele ya macho yetu. Tuwe na kiasi katika kila jambo.
Maoni
Ingia utoe maoni