Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Februari 18, 2022

Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Februari 18, 2022,
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa

Mk 8:34 – 9:1.


KUMFUATA YESU!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Mt. Yakobo anazungumzia juu ya umuhimu wa matendo katika imani. Imani ya Mkristo lazima akoleze maisha yake kwa matendo mema. Yesu alipofanya utume wake duniani, aliunganisha mafundisho yake na matendo mema. Hakuhubiri kwa maneno tu. Yakobo alitaka imani ya Ukristo ieleweke kama imani inayopaswa kugusa maisha ya kila mmoja katika jamii. Ukristo hutufanya tuwe ndugu kwa kila mmoja na kumpenda kama tunavyojipenda wenyewe. Na hili lazima lionekane katika matendo pia.
Wakristo wa kipindi cha Yakobo walikuwa katika mahangaiko makubwa ya kiuchumi na baadhi ya wakristo walipokuwa wanawatembelea wakristo wenzao-hasa waliokuwa wagonjwa, wapo waliokwenda kwa mikono mitupu na kuwapatia maneno matupu tu. Yakobo anataja kwamba pepo ndio wenye maneno mengi. Baadhi ya pepo walikiri kwa maneno kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu bila ya wao wenyewe kumwamini. Yakobo anataka wakristo kuepuka kuwa watu wa maneno mengi-hizi ni tabia za pepo wachafu. Waone shida za wenzao. Waachane na ubinafsi wa kuficha rasilimali zao na kuwaacha wakristo wenzao katika ugumu.
Walipaswa kufuata mfano wa Ukarimu wa Abrahamu, ukarimu wa Yakobo na ukarimu wa Isaka. Kwa ukarimu wao waliweza hata kuwakaribisha hata malaika bila kujua. Wakristo hawapaswi kuona wakristo wenzao walio katika shida kama mzigo, wanapaswa kuona sura ya kimalaika ndani ya mioyo yao pia. Hivyo sio kila maskini unayemhudumia kuwa ni mzigo. Mwone kama malaika. Wenzetu wanayo sura ya Mungu ndani ya maisha yao.
Yesu katika injili anaelezea juu ya umuhimu wa kumkiri yeye hasa mbele ya watu itamfanya na yeye apate kumkiri mbele ya Mungu na malaika wake. Somo hili litusaidie na sisi tuachane kuwa na tabia za kisaliti, usaliti hasa wa imani yetu. Mara nyingi tunamsaliti Yesu katika sehemu tulizoajiriwa, pale tunapoanzisha urafiki na wenzetu ambapo tunaruhusu watushawishi katika kuikana imani yetu.
Tuepuke kuwa watu wa tamaa, turidhike na kila kidogo tulichopewa. Hili litatusaidia kuridhika na kuepuka kuingia katika matendo, biashara na taaluma na burudani zenye kuikana imani yetu. Wapo kati yetu ambao ni wakristo lakini kwa sababu ya tamaa ya fedha, au madaraka, au anasa tunakuwa tayari kujihusisha na biashara za night clubs, usafirishaji haramu wa wanadamu, kushiriki katika biashara za utoaji mimba na uuzaji na utengenezaji wa filamu mbaya na website mbaya. Hapa ni kumkana Yesu hadharani. Kila mmoja wetu ajitahidi leo achunguze shuhguli yake anayofanya na kuona kwamba haiongozwi na tamaa au maadili mabaya.

Maoni


Ingia utoe maoni