Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 16, 2022

Jumatano, Februari 16, 2022,
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa

Mk 8: 22-26.


HATUA MOJA MBELE!

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili leo, Bwana Yesu anafungua macho ya kipofu. Kipofu huyu aliletwa kwa Yesu na baadhi ya watu wa kijiji cha Betsaida ili apate kuponywa. Yesu anamponya na mwishowe anaweza kuona kwa usahihi kabisa. Watu waliomleta kipofu huyu kwa Yesu hakika walikuwa ni watu wenye nia njema na kipofu huyu. Walimpenda, walielewa mateso yake, wakatambua ni wapi wampeleke ambapo atapata msaada. Na kwa hakika kipofu anapata msaada bora kabisa.
Sisi tuige mfano na roho ya hawa waliompeleka kipofu kwa Yesu. Tunapaswa kuwapeleka wenzetu kwa Yesu. Wapo wengi wenye matatizo kuliko kipofu huyu na wanasumbuka kupata eneo la kwenda. Wengi wanatafuta kuponywa magonjwa kama ya kansa, wengi wanatafuta wachumba, wengi wanatafuta kazi, na wengi wanafuta faraja maishani mwao. Shetani anawakamata kirahisi wengi wenye kukumbwa na shida za namna hii kwa sababu ya kukosa maarifa ya wapi wapeleke shida zao. Hivyo tuwapeleke wenzetu wote kwa Yesu kama walivyofanya wanakijiji wa leo.
Pia tujifunze kusikiliza maumivu ya wenzetu na tunyanyuke kuwasaidia kama walivyonyanyuka watu wa kijiji hiki. Tunyanyuke tuwapeleke wagonjwa wasio na uwezo hospitalini, tunyanyuke tuwapeleke watoto wa familia zisizo na uwezo shuleni. Bwana Yesu ni mwenye uwezo mkubwa. Aliweza kuyafungua macho ya kipofu huyu na kuweza kuona katika ukamilifu wote. Sisi tusisite kumkimbilia Bwana Yesu.
Kwenye somo la kwanza, Mt. Yakobo anazungumzia kuhusu umuhimu wa matendo katika imani ya Mkristo. Mkristo asiwe mtu wa maneno tu, anapaswa kuwa pia mtu wa matendo, imani yake bila matendo haiwezi kuleta mabadiliko aliyoyatangaza Yesu. Dini ya kweli lazima ihusike na maskini, vilema, viwete, na watu mbalimbali walio na shida. Hakika hatuwezi kujiita wafuasi bila kutekeleza matendo haya. Hivyo mkristo asiache kabisa kutenda matendo ya huruma. Haya ndiyo yatakayokoleza ufuasi wake na kuwa na utume bora kwenye eneo lake.
Jumuiya isiyotenda matendo mema ni Jumuiya ya kibinafsi isiyo na chachu ya kuleta mabadiliko katika eneo iliyopo. Sehemu zote ukristo ulipoendekeza ubinafsi ukristo umeishia kuleta ushawishi kwa watu. Tunapaswa kuondokana na ubinafsi ili tuweze kuwa chachu ya mabadiliko kwa wenzetu.

Maoni


Ingia utoe maoni