Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Februari 10, 2022

Alhamisi, February 10, 2022
JUMA LA 5 LA MWAKA

1 Fal 11:4-13;
Zab 106:3-4.35-37.40
Mk 7: 24-30.

KUDHIHIRISHA IMANI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika neno la Bwana tunaanza kwa kuliona somo la kwanza ambapo tunakutana na kibao cha ajabu. Jana baada ya kusikia kwamba Solomoni alikuwa na hekima za ajabu hadi watu kutoka mbali wakaja waone hekima yake, Solomoni akasifika, akaonekana kama mtu aliyebarikiwa na Mungu, leo hii tunasikia kitu cha ajabu. Anapoteza hekima ile na tunasikia Mungu akimtangazia adhabu-anatangaza kumnyanganya ufalme. Japokuwa alikuwa na hekima kubwa-anawasababishia wana wa Israeli mateso makubwa. Hii ni habari ya kusikitisha. Na ndugu zangu kilichomletea yote haya ni dhambi. Yeye aliacha kusikiliza mwongozo wa Mungu akafuata mwongozo wa wake zake, wake zake wakawa na sauti kuliko Mungu, wakamshawishi kwenda kuiabudu miungu mingine. Jana tuliona kwamba hekima inapatikana kwa kumtii Mungu. Mtu anayesali hata kama hajasoma anakuwa na hekima tu, asiyesali hata kama ni profesa huwa anakuwaga ni majanga. Solomoni kilichompotezea hekima ni kutomtii Mungu. Na cha ajabu ni kwamba Solomoni haombi msamaha kama Daudi alivyoomba. Hekima zake zimekuwa ni sifuri. Angeomba msamaha angesamehewa na Mungu. Kwa kweli solomoni kabadilika.

Ndugu zangu, kuanguka kwa Solomoni ni mwamba umeangushwa, ni kama sisimizi amemwangusha Tembo na hivyo Tembo anachekwa sana. Tembo unakutwa alikuwa anategemewa aonyeshe nguvu zake na hakutegemewa ashindwe na sisimizi. Laikini imetokea. Na hii ni aibu kubwa-sasa tembo ajifiche wapi? Nasi ndugu zangu, sisi yabidi tujifunze kitu. Kuna sehemu ambazo twaweza kuanguka lakini baadhi ya sehemu zitatupatia fedheha kubwa. Na hii itatokea pale ambapo umeangushwa na kitu cha ovyo au kitu ambacho kila mtu asingetegemea kikuangushe na huu unakuwa wakati wa aibu na waweza hata kuomba ardhi ipasuke. Tuombe Mungu kila wakati ili nyakati kama hizi zisitokee na zikitokea tuzidi kumkimbilia yeye bila kukata tamaa. Tusiwe kama Solomoni aliye kataa kuomba msamaha.

Somo la injili twakutana na mama mmoja anayetafuta uponyaji. Yesu anatumia maneno makali kwake na kinachomwokoa ni kwamba yeye alikuwa na imani, na Yesu anampenda. Yesu alitaka kuona imani ya huyu mama isije ikawa kwamba huyu mama alimuona Yesu kama mwana mazingaumbwe au mpiga ramli. Hivyo, kwa Imani yake aliikoa nafsi ya mtoto wake lakini kwa kukosa imani kwa Solomoni, alilitea taifa madhara.

Ndivyo ilivyo ndugu zangu kwa yeyote anayetegemewa halafu akaishia katika upotofu. Yeye huwaangusha wengi. Hata baba ndani ya familia au padre au hata kiongozi wa serikali. Jua kwamba unategemewa. Ujinga wako kidogo tu unawaletea wengi madhara makubwa. Unakuwa ni sababu ya taifa zima kuishi labda katika umaskini, au baba kwa ujinga wako unakuwa sababu ya watoto wako kuishi katika umaskini. Tumuombe Mungu atupe imani kama Mama huyu ili tuweze kuwasaidia wengi

Maoni


Ingia utoe maoni