Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Februari 12, 2022

Jumamosi, Februari 12, 2022
Juma la 5 la Mwaka wa Kanisa


1Fal 12:26-32;13:33-34
Zab 106:6-7.19-22
Mk 8: 1-10.

JE UNA NJAA YA MUNGU?

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na habari za yanayofuata baada ya ufalme wa Israeli kugawanyika mara mbili baada ya kifo cha mfalme Sulemani. Mungu anampatia Jeroboam kutawala makabila 10 ya Israeli. Na anapoanza kutawala cha kwanza anachokifanya ni kuwanyima watu kwenda kuhiji katika hekalu la mji wa Yerusalemu-anaamua kutengeneza sanamu mbili na kuziweka katika miji ya Dan na Bethel na kuagiza ziabudiwe na kutolewa uvumba na sadaka. Kosa analolitenda Jeroboam ni kumfananisha au kumlinganisha Mwenyezi Mungu, Bwana wa Israeli, anamlinganisha na sanamu, anafikiri kwamba sanamu inaweza kulinganishwa na Bwana Mungu.
Pia alifikiri kwamba mji wa Yerusalemu uliochaguliwa na Bwana kuwa kikao chake unaweza kulinganishwa na mji wa Dan au Bethel. Kwa kosa hilo aliyapotosha makabila yote kumi ya Israeli kwani kilitokea kizazi ambacho kilishindwa kutofautisha kati ya sanamu na Bwana Mungu wa Israeli na hivyo kuishia kuabudu sanamu kama ilivyokuwa kwa mataifa jirani.
Sisi tuepuke kufanya mambo yanayofanana na yanayotendwa na Jeroboam. Hata siku moja tusilinganishe mambo ya Bwana. Bwana hawezi kulinganishwa na chochote. Bwana apewe Bwana. Ukijaribu kumfananisha Mwenyezi Mungu na chochote kilicho katika ulimwengu mara nyingi utaishia kumwabudu Mungu aliye tofauti. Mwenyezi Mungu halinganishwi. Kama ni siku ya Bwana ya kusali jumapili, basi siku hii iheshimiwe kipekee na utakatifu wake utunzwe. Isije ikachukuliwa kama siku ya kawaida ya kazi za kawaida, mwishowe tutapoteza utakatifu wake kwetu kama Jeroboam alivyochukulia hekalu na mji wa Yerusalemu kuwa kitu cha kawaida na mwishowe watu wakaishia kutokutambua utakatifu wa mji huo na hekalu lake.
Pia tuepuke kulinganisha sakramenti zetu na chochote. Kulinganisha matakatifu na chochote ni chanzo cha kupotea kiimani. Matakatifu yasilinganishwe na chochote. Kumchukulia Mungu kuwa kama mganga flani wa kienyeji ni kosa, yeye ni zaidi ya yote. Hii haina maana wale wanaotumia picha au sanamu kumtafakari Mungu wanakosea hapana, kama kitu hakikufanyi umkumbuke Muumba mwenyewe ni mbaya ila kama kama kinakusaidia kumtafakari Mungu zaidi ni vyema.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anawalisha makutano aliokaa nao chakula. Makutano haya alikaa nao kwa siku tatu na mwishowe amewafanya kama rafiki na hakubali kuwaona wakiondoka katika njaa ili wakafie njiani. Yesu hataki urafiki wake na makutano haya uishie kwa siku ile ile. Anataka udumu zaidi na anawapa chakula kitakachowapatia uhai.
Anapowapa chakula Yesu anachukua kile kidogo kilicho kwao na kukibariki na kuwapa na wengi wanapata kula na kushiba. Yesu anatufundisha kuonesha urafiki wa kweli kwamba usiwe wa maneno tu bali wa vitendo. Tutimize shida zao. Wengi wetu tumezoea urafiki wa kupiga domo na kuwapiga watu Kiswahili kirefu tu. Tuwe watu wa matendo. Na pia tujiandae kutoa tulichonacho na ndipo sisi wenyewe na wenzetu tulio nao watakapoweza kula na kushiba kama alivyofanya Yesu leo.
Tukificha kile tulichonacho kwa hakika tutashindwa kuwafanya wenzetu wapate kushiba na sisi wenyewe tutajizuia kushiba. Tuwe tayari kutoa kile tulichonacho na ndipo na sisi tutakapoweza kushiba.

Maoni


Ingia utoe maoni