Jumanne, Februari 08, 2022
FEBRUARI 8, 2022
JUMA LA 5 LA MWAKA
1Fal 8:22-23.27-30
Zab 84:2-4.9-10
Mk 7: 1-13.
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linaanza kwa kusisitizia juu ya furaha yenye kupatikana katika hekalu la Bwana. Tukiichambua Zaburi yetu ya wimbo wa katikati leo, tunagundua kwamba mwenye kuiandika zaburi hii kwa hakika aliiandika kwa hisia nzito kwani inaonekana kwamba alikaa muda mrefu bila kuwa karibu na hekalu, alikaa kati ya watu wakatili, sehemu zisizo na amani, sehemu zenye kukosa roho ya sala.
Anayeimba Zaburi hii anadiriki hata kumwonea shomoro wivu-ndege aliyeweka kiota chake karibu na madhabahu ya Bwana. Yeye anatamani angalau kama angekuwa huyu shomoro, au hata aruhusiwe kukaa muda wote kwenye viwanja vya hekalu. Mwenye kuimba zaburi hii alikuwa Myahudi aliyekuja kuhiji hekaluni baada ya kukaa muda mrefu sana nje ya Yerusalemu.
Wayahudi wengi waliishi katika miji ya Alexandria na huko walikumbana na falsafa na maadili maovu ambavyo havikuilisha roho zao. Mt. Augustino anafundisha kwamba moyo wa Mwanadamu hautulizwi na pombe, au kisomo au falsafa bali hutulizwa na Bwana.
Zaburi ya leo itufundishe kuilisha mioyo yetu kwa sala, neno la Mungu na matendo mema. Tusiache kusali au kusoma neno la Mungu hata tukiwa katika changamoto na matatizo mbalimbali kama ya kufeli mitihani na misiba mbalimbali. Tusigeukie faraja za kwenye vinywaji vikali au madawa ya kulevya.
Mfalme Solomoni katika somo la kwanza leo anatufundisha kwamba hekalu ni mahali alipopachagua Bwana ili apate kuabudiwa. Kati ya maeneo yote, Solomoni alimwomba Mwenyezi Mungu akubali kukaa hekaluni, naye Bwana alikubali ombi hili. Nasi tupendelee kufika maeneo ya kanisa na kusali. Wapo tunaojivuna na kusema kwamba Mwenyezi Mungu yupo kila mahali hivyo naweza kusali popote. Lakini tutambue kwamba Mungu amechagua mahali anapopenda aabudiwe. Hivyo, tunaowajibu wa kuja kanisani kusali. Tuache tabia za kutokuhudhuria misa na wenzetu.
Yesu katika somo la injili anahuzunika kwa kitendo cha mila na desturi za kiyahudi kupewa kipaumbele kuliko imani na mafundisho sahihi ya dini hiyo. Wanadamu wanayotabia ya kutetea ya kwao kuliko kutetea ya Mungu. Sisi tuwe makini sana na imani yetu. Tuhakikishe kwamba ubinadamu hauingilii maisha yetu ya imani. Tusiruhusu tamaduni zetu hasa za kiasili na za utandawazi kuonekana kwamba ni juu zaidi ya sakramenti zetu. Kristo anapaswa kutawala tamaduni zetu. Moyo ulio najisi ndio mbaya zaidi.
Maoni
Ingia utoe maoni