Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 09, 2022

Jumatano, Februari 9, 2022
Juma la 5 la Mwaka

Mk 7: 14-23.


NDANI NA NJE!

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi ya wimbo wa katikati linatupatia ujumbe kwamba kinywa cha mwenye haki huongea maneno ya hekima. Na kwa hakika mawazo yake na nia zake huwa njema.
Hii ni kwa sababu ya uwepo wa Roho wa Bwana mwenye kumfundisha.
Maneno ya hekima ni maneno safi, maneno yenye kuleta faraja palipo na magumu, yenye kutuliza, yenye maarifa. Bwana humfunza maarifa yeyote aliye na haki na nia njema. Zaburi hii inatumika kusisitizia maisha ya Solomoni. Yeye alipokuwa katika kumcha Bwana na kutenda haki, hakika alipata hekima kubwa, alipata maarifa ya kuongoza nchi yake na mawazo ya kusema. Wafalme kutoka mbali walifunga safari kuja kumwona ili kujifunza hekima kwake. Hii ni kwa sababu alimcha Bwana.
Nasi tupendelee kutenda mema na kumcha Bwana. Huu ndio msingi wa hekima. Hakuna mwenye hekima na wakati huo huo ni mwovu au mtapeli. Hekima huambatana na utendaji wa haki. Hivyo tutambue kwamba tutajipatia hekima na maarifa mengi kwa kutenda haki. Tusiache kutenda mema.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anazidi kusisitizia juu ya faida iliyopo kwa pale tunapotenda matendo mema. Anaonesha kwamba matendo mema na mawazo mazuri ndiyo yenye kumfanya mtu angae na kupendeza na sio kile anachokula mtu.
Yesu anatoa maneno haya kwa sababu Wayahudi wengi waliweka msistizo kwenye chakula na usafi kuliko mawazo yaliyomo moyoni mwa mtu. Walifikiri kwamba chakula na usafi kina uwezo wa kumfanya mtu kuwa najisi kuliko mawazo, maneno na matendo yake. Injili hii itufundishe na sisi leo. Wapo kati yetu ambao hasa kwenye siku za sikukuu kubwa za kanisa tunajiandaa kimwili zaidi kuliko kiroho. Roho zetu mara nyingi hutelekezwa na kuusafisha zaidi miili yetu. Tujifunze kuweka msisitizo kwenye roho zetu pia.
Pia tuwe watu wa kuwafikiria wenzetu mawazo mema. Mawazo mabaya ninayomwazia mwenzangu mara nyingi ndicho kikwazo kinachonifanya mimi mwenyewe nishindwe kusonga mbele. Sisi tusiache kuwawazia wenzetu mema. Hapa ndipo kuwa na moyo mzuri na mwema.

Maoni


Ingia utoe maoni