Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Februari 07, 2022

Karibuni sana ndugu wapendwa kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, tunaelezwa kwamba watu wa nchi ya Genesaret, waliofanikiwa kunyanyuka na kumgusa Yesu, waliofanikiwa hata kugusa pindo la vazi lake walipona. Wengi walijitahidi kufanya haya na kupata uponyaji. Hakika ndivyo alivyo Bwana. Ni mwenye uwezo mkubwa. Hata pindo la vazi lake laweza kutoa uponyaji. Lakini pindo hili lazima liguswe kwa imani.

Ukweli ni kwamba nyakati za Yesu, walikuwapo wengi waliomgusa lakini sio wote waliopona kwa sababu wengine hawakumgusa kwa imani.

Hata nyakati zetu, wapo wengi tunaokutana na kumgusa Yesu katika Ekaristi lakini wanaoponywa au kupatiwa faraja ni watu wachache tu. Hivyo tunaposikia habari za nguvu kuu za Yesu zenye uwezo wa kupatikana mpaka kwenye upindo wa vazi lake, tujifunze sisi wenyewe kuwa na imani, tujihuzunikie kwa pale tunapomkosea Yesu adabu, tunapoona aibu kumgusa kwa imani katika Ekaristi na katika neno lake. Tukumbuke kwamba Yesu ni uwezo wote, lakini wengi wetu hatujawa na imani ya kulitekeleza hili ndani ya maisha yetu. Maisha yetu yote yafanane na ya hawa watu wa Genesareti wanaokazania kumtafuta Yesu. Maisha yetu nasi yamtafute Yesu.

Wapo tunaotumia muda mrefu kuwatafuta marafiki tutakaofanya nao maovu. Hapa ni kujididimiza kimaendeleo. Tutafute kumgusa Yesu.

Katika somo la kwanza, Mfalme Solomoni analeta sanduku la agano ndani ya hekalu la Yerusalemu. Mfalme Solomoni amefanikiwa kumjengea Bwana hekalu na leo anamkabidhi Bwana hekalu hilo kwa kuamua kulileta sanduku hilo ndani ya hekalu hili. Bwana anakubali kukaa ndani ya hekalu hili na kwa hakika mji wa Yerusalemu utapata baraka nyingi kwa uwepo wa hili hekalu.

Nasi tumwige mfalme Solomoni katika kuleta matakatifu ndani ya nyumba zetu na makazi yetu. Tulete vitabu na visakramenti ndani ya makazi haya. Tusikubali kuleta mikanda ya filamu mbaya, marafiki wabaya au kuruhusu tabia ovu za ulevi na uasherati zifanyike katika makazi yetu. Haya ni chanzo cha laana kwetu na kukosa baraka toka kwa Mwenyezi Mungu.
Tujifunze kupendelea matakatifu.

Pia tujifunze kuwaita mapadre wabariki maeneo ya kazi na hivyo kumleta Roho wa Bwana atawale maeneo haya kama anavyofanya Solomoni.

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni