Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Februari 05, 2022

Jumamosi, Februari 5, 2022,

Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa

1Fal 3:4-13
Mk 6: 30-34.

YESU MWENYE HURUMA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na mfalme mpya aitwaye Solomoni, ndiyo anaanza ufalme wake. Sasa kabla ya kuanza ufalme wake, kabla mambo hayajaanza kukolea ndani ya ufalme wake, anaanza kwa kwenda mbele ya Bwana na kuomba hekima. Anaamua kwenda Gibeoni kutoa dhabihu, kumshukuru Mungu kwa kumpatia ufalme na kumuomba Mungu aubariki ufalme huo ili angalau mambo yaende vizuri ndani ya huo ufalme wake. Hivyo, aliaanza kwa kukaa na Bwana na kuomba msaada na maongozi mbele ya Bwana.

Tukija katika Injili, tunakutana na kitu kama hicho hicho lakini hapa ni wale wafuasi ambao juzi tulisikia wakitumwa na Bwana kwenda kutangaza ufalme wa Mungu. Sasa leo wanarudi kwa furaha. Yesu anapowaona tu-tena wakiwa katika furaha zao, yeye anasema basi, njooni hapa, mahali pasipokuwa na watu ili tukae, tuyaongee haya mambo, tuelezane jinsi huo utume ulivyokwenda. Lengo la Yesu hapa lilikuwa ni wao watoe mwenendo mzima jinsi kazi yao walivyoiongoza. Labda hawa wafuasi wangeishia katika kufikiri kwamba mafanikio ya utume ni watu wengi kukusikiliza, labda ni kutoa pepo wengi, labda ni kukaribishwa na watu vizuri, labda ni kuheshimika NA KUITWA RABI AU MASTA ni kweli hawa wafuasi wangeweza kuishia kuwa na mawazo ya namna hii.
Lakini Yesu inabidi akae nao, wachunguze utume wao wote, awaeleze hali halisi ya nini maana ya utume. Hiki kilikuwa ni kitu cha muhimu sana ili wasije wakawa na maana potofu kuhusu ufalme wa mbinguni na utume. Na walipokuwa wanatafuta nafasi hii makutano walikuwa wanakazana kuja, kuwatafuta hata wasiipate hii nafasi lakini tunaona kwamba Yesu alikazana kuhakikisha kwamba ameipata hii nafasi na ndipo baadaye alipowajia.
Ndugu zangu, hapa twajifunza kitu. Lazima kutenga muda na kutathmini shughuli zetu tunazofanya-lazima kutenga muda kutafakari maisha yetu ya Kikristo. Bila hili, huwezi kusonga mbele ndugu yangu. Ukitenga muda wa kujichunguza, unapata kutambua sehemu uliyokosea, wapi unahitaji marekebisho, wapi uombe msaada. Wanaofanya hivi hufanikiwa na ndio maana kwa watawa/Mapadre wanavyo vipindi vya ritiriti-wanayatathmini maisha yao ili wasonge mbele na kujifanyia marekebisho na kuanza tena upya. Hapa unapata nguvu na mbinu mpya za kushinda vishawishi vya muovu na kusonga mbele.
Kipindi chetu ndoa nyingi zimevunjika, watu wengi wameacha hata maisha ya utawa, watu wamevunjiana urafiki, kutukanana, kununiana kwa sababu ya kukosekana kwa kipindi cha tathmini kuhusu maisha yao. Hivyo, tutambue umuhimu wa kipindi hiki. Hiki kitatufanya tusonge mbele.

Tumsifu Yesu Kristo.....

Maoni


Ingia utoe maoni