Jumapili, Februari 06, 2022
Februari 6, 2022
DOMINIKA YA 5 YA MWAKA WA KANISA
VILIVYO VIDHAIFU KUPEWA THAMANI YA KUMTANGAZA MUNGU
Jumapili iliyopita tulisikia kuhusu wito wa Yeremia, na leo tuna habari tena ya wito wa Isaya na Petro. Mmoja anaweza kujiuliza kwanini Mungu anachangua watu kama hawa? Mungu anafikiria nini? Lakini ukweli ni kwamba hili sio jambo geni kwa Mungu. Abrahamu alichaguliwa na Mungu akiwa mzee ili awaweze kuwa Baba wa taifa la Israeli, Mungu alimchagua Musa ambaye alikuwa hawezi kuongea vizuri, kigugumizi ili kukabiliana na Farao na kuongoza wana wa Israeli, Kijana mdogo tena mchungaji, Daudi alichaguliwa na Mungu kuwa Mfalme wa Israeli. Na pia Sauli ambaye alikuwa mtesi wa Kanisa anachaguliwa na Yesu kuwa chombo chake kiteule cha kuhubiria Injili yake. Hii yadhihirisha kwamba Mungu anafanya kadiri ya mapenzi yake.
Vyombo anavyo vichagua Mungu ni kutoka katika ulimwengu wetu, hata kama sisi tunaviona ni dhaifu. Tunaweza tukakosea sana na kudhani kwamba sisi hatustahili kuwa wafuasi wa Mungu. Mungu amewachugua watu wengi kama wewe na mimi kuwa wafanyakazi wa shamba lake.
Baada ya muda mrefu wa kuvua samaki, Yesu anamchagua Petro sasa aweze kuwa mvuvi wa watu. Petro anatambua kutokustahili kwake. Lakini anatambua kuwa Yesu amemchagua kwa ajili ya kazi yake kubwa licha ya udhaifu wake. Na kuanzia sasa atakuwa mvuvi wa kuwaleta watu katika jarife la Mungu. Lengo la Mungu kwetu sisi halitegemei kustahili kwetu. Ile hali yetu yakujiona hatustahili inatufanya tuwe tayari kufanya kazi na Yesu. Sisi tukiwa kama Petro tutafanya kama yeye huku tukijaribu kuishi kile tunachohubiri.
Tuombe neti ya Mungu inaporushwa duniani kwa njia ya habari njema iweze kutuvua na kutupeleka kwake. Kwa Mungu kuna huruma na Upendo, pamoja na madhaifu yetu bado tuna hakika tunapoenda kwa Yesu tunakutana na huruma na upendo. Pamoja na kutokustahili yetu, bado kuna tumaini la kustahilishwa na Yesu mwenyewe. Tunapaswa kujitoa sisi wenyewe kurusha hii neti ya Mungu duniani pia ili tuweze kuwavua wengi na kuwaleta katika ufalme wa Mungu. Sisi kama Petro tunaitwa kuwa wavuvi wa watu.
Pengine maisha yetu tumeyaishi bila kufanikiwa na tupo katika hali ya juu kabisa ya kukata tamaa kama Petro ambaye hakuwa amevua hata samaki mmoja. Sisi tukimbilie kwa Yesu, yeye atayarudishia thamani maishsa yetu. Tuwe wanyenyekevu tujishushe na kujiona hatustahili ili Yesu mwenyewe atusatahilishe. Tukijishusha yeye atatunyanyau juu zaidi. Tuombe neema hiyo ili tuweze kustahilishwa na Yesu.
Sala:
Bwana Yesu umeniita katika wito huu kama Mkristo ili niweze kukushuhudia kwa maisha yangu, pengine maisha yangu hayajavua au kumvutia yeyote ili aje kwako. Nakuomba unipe neema ya kuweze kukuishi ili niweze kuwa chombo cha kuvulia watu kwa njia ya maisha yangu, sikuombi uondoke kwangu bali nakuomba ukae kwangu.
Amina.
Maoni
Boniface Mwema
Tafakari nzuri. HongeraIngia utoe maoni