Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Januari 25, 2022

Januari 25, 2022

JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA

2Sam. 1:1-4, 11-12, 17, 19, 23-27
Zab. 80:1-2, 4-6 (K) 3
Mk 3: 20-21

VIPINGAMIZI KATIKA KUMFUATA YESU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo ni siku ya uongofu wa mtakatifu Paulo. Habari za jinsi alivyoongoka tunazipata katika somo la kwanza. Na tunaona kwamba Uongofu huu ni wa ajabu kabisa na hapa ndipo tuwezapo kushuhudia kwamba kweli neema ya Mungu inatenda kazi. Kama hujawahi kuisikia juu ya neema hii au kuiamini, huwa nikisikia kilichomtokea Paulo lazima niamini tu. Ni mtu anayekuja kuwa askari na mtetezi hodari kuliko hata wale waliomtangulia mwanzo wa kile kitu ambacho yeye mwenyewe alikichukia hapo kwanza. Na kwa njia ya huyu Mtakatifu, watu wengi wamekuja kwa Kristo hasa sisi watu wa mataifa. Kweli neema ya Mungu inafanya kazi.
Katika injili, tunasikia wale kumi na mmoja wanavyotumwa na Yesu na wanapewa ishara zitakazoambatana nao. Mojawapo ni ya kushika nyoka bila kuwadhuru. Hii ilitokea kwa Paulo mwenyewe katika Biblia. Yeye ndiye aliyeshika nyoka mkali mwenye sumu na kugongwa na yule nyoka lakini hakuanguka au kufa (Mdo 28:3-6). Kweli Kristo alikuwa pamoja naye.
Mtakatifu huyu baada ya uongofu wake na kujua kile alichotakiwa kufanya, kama vile Mtakatifu Francisko wa Assisi alivyoongozwa na Bwana, yeye alikuwa mpole na mwaminifu na kufuata kile alichoambiwa na Bwana. Alitii kwa uaminifu na hakuna chochote alichokifanya bila kuomba msaada wa Mungu. Alikuwa mpole mbele ya mapenzi ya Mungu. Hata nabii Agabus alipomtabiria juu ya kifo chake wakati atakavyoenda Yerusalem na kupelekwa gerezani, hata wale Wakristo kulia baada ya kusikia hivyo na kumsihi Paulo asiende, yeye alikipokea kifo hiki kama mapenzi ya Mungu. Hata siku moja hakukikataa au kupinga mapenzi ya Mungu.
Ndugu zangu Mtakatifu Paulo ni funzo kwetu. Sisi haimaanishi kwamba Yesu au Mungu kakataa kuzungumza nasi siku hizi. Ukweli ni kwamba Mungu huzungumza nasi. Lakini shida ni kwamba watu sio watii au wapole kama Paulo alivyokuwa. Watu wanajiona ni wajuaji na watu tunatafuta mno maslahi. Kitu kidogo tu lakini umeshatafuta maslahi, unakimbia maongozi ya Mungu.
Neema ya Mungu ipo kila wakati lakini tunakosa ushirikiano nayo, hii ndiyo shida ndugu zangu, tungekuwa kama Paulo, nakwambia ungekuta tuko mbali sana, nakueleza, hivyo, embu tuoneshe utii leo kwa neema ya Mungu na nakwambia tutaona mengi. Hakika nakuambia. Tutaona mabadiliko makubwa maishani mwetu ndugu zangu.
Wengi wetu tumeshajizuia sana kumfanya Mungu ashindwe kutubadilisha. Tumemzuia, hatumpi nafasi, tunataka tufuate yetu. Hii ni hatari.Tunapotumia muda kuangalia visimu vyetu tu, kuangalia vivideo mbalimbali au kufuatilia vipindi mbalimbali na kuacha tafakari juu ya uhusiano wako na Mungu, sala hazitukutanishi tena pamoja lakini Tv inatukutanisha kwa ajili kuangalia tu nakuondoka, utasikia sauti ya Mungu saa ngapi? Tuwe na kiasi ndugu zangu, tusiibe nafasi ya Mungu-nakwambia itatufanya tuishie pabaya tu. Tuige mfano wa huyu mtakatifu.

Maoni


Ingia utoe maoni