Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Januari 24, 2022

January 24, 2022
JUMA LA 3 LA MWAKA

2sam 5:1-7.10
Zab 89:19-21.24-25
Mk 3: 22-30.

KUACHA DHAMBI



Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Leo katika neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunamsikia Daudi akifuatwa na wazee wa Israeli akiombwa awe mfalme juu ya taifa nzima la Israeli. Hii ilitokana na uaminifu wake na alivyoonekana kuwa mtu wa haki na namna jinsi alivyojitahidi katika kuwaunganisha watu na jinsi alivyokuwa na moyo mwema juu ya taifa nzima la Israeli. Hivyo, walimfuata na kumwomba awe mfalme wa taifa nzima.
Hapa, wana Waisraeli wanakuwa wakweli na wanamtukuza Mungu kabisa kabisa-na Mungu anatukuzwa katika Daudi kwani kwa kazi nzuri ya Daudi, watu wameona na kutoa ushuhuda. Katika somo la Injili, tunakutana na kitu tofauti kabisa. Yesu anaponya na badala ya watu kumfurahia na kumpongeza, wao Wafarisayo wanasema ati kaponya kwa kutumia Beelzebul, yaani badala ya kuona kazi nzuri na kumtukuza Bwana kama wana wa Israeli walivyofanya, wao waliona kazi nzuri ya Bwana na kumtukana Yesu, na kuona kwamba Beelzebul ana nguvu na wema mwingi hata kumshinda Yesu, wakaona kwamba Beelzebel ni wa muhimu kuliko Yesu.
Yesu anawaambia kwamba yeyote atakayemkufuru Roho mtakatifu, hatasamehewa. Hii yamaanisha kwamba yeyote yule ambaye ataona matendo makuu ya Mungu kihadharani hivyo kama Yesu alivyofanya halafu yeye akaacha kumtukuza Mungu na kumtukuza shetani, hakika huyo atakuwa na jambo kubwa, kesi kubwa ya kujibu. Huyo hatasamehewa. Yesu kajitahidi, kaja kwako kwa hali zote, kajishusha kwako kila wakati kukuonyesha ukuu wa Mungu na wewe unauacha, nakwambia hutasameheka.
Hili ni fundisho kwetu ndugu zangu. Mungu anapokazana na kukuonyesha matendo makuu ya kwake, akikutaka uongoke, na wewe kubali, usikatae kile anachokuletea akitaka ubadilike. Nasi tuone matendo makuu ya Mungu na kubadilika. Usiyaone na kumtukuza shetani zaidi. Huu ni ukosefu wa heshima, ni kudharau nguvu za Yesu anazotuonesha kila siku ndugu zagu. Ni kama kuungata mkono wa Yesu unaokuja kwako ukikutaka kukuinua katika matope na wewe unaona ni afadhali nibaki katika haya matope. Hivyo, tujifunze kuwa wapole na siku zote tayari kujitolea kwa jili ya Kristo na kumfanya atukuzwe.

Maoni


Ingia utoe maoni