Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Januari 19, 2022

Jumatano, Januari 19, 2022.
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa

1Sam. 17:32-33, 37, 40-51
Zab. 144:1-2,9-10 (K) 1
Mk. 3:1-6

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuh ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunasikia habari za Goliathi, askari mkubwa na shujaa wa Kifilisti akishindwa na Daudi. Kushindwa kwa huyu askari kulikuwa jambo la kufedhehesha kwa yeye mwenyewe na taifa lote la Kifilisti kwani askari huyu alishindwa vibaya na kijana mdogo kabisa ambaye hakuwa hata na uzoefu mkubwa wa vita.
Na kitendo cha Goliathi kushindwa kulilifanya taifa lote la Wafilisti wakimbie na Waisraeli kupata nguvu ya kuwakimbiza Wafilisti na kuwashinda vita. Hakika Goliathi aliuumbuka kwani alikwenda akijiamini mno, aliamini uzoefu wake, misuli yake na silaha zake. Lakini leo vinashindwa kabisa. Goliathi alimtukana Bwana Mungu wa Israeli akitegemea kwamba nguvu zake zitamwezesha kushinda.
Sisi nasi tuogope kuwa kama Goliathi, tusiwe watu wa kutegemea nguvu zetu na kumwacha Mwenyezi Mungu. Kila asubuhi ukiamka mkumbuke Goliathi anavyoangushwa leo na hivyo tuwe wanyenyekevu na kumwambia Mwenyezi kwamba hata kama nina akili, hata kama nina uwezo na nguvu na afya kiasi gani, najua naweza kushindwa na kijana mdogo kama Daudi. Hata kama ni biashara au darasani au pesa waweza kushindwa na kijana mdogo kabisa. Hivyo naomba unilinde. Nisije nikafedheheka kama Goliathi alivyofedheheka.
Pia tuachane na tabia ya kuwaonea wadogo. Kila unayemwonea nayeye kumlilia Mungu kama Daudi alivyomlimlia Mwenyezi Mungu, jua kwamba utafedheheshwa vibaya sana kwani nguvu zako na cheo chako vitayeyuka vyote kama Goliathi anavyoyeyuka kwa siku ya leo. Tujifunze kumlilia Mwenyezi Mungu, kwani Mungu humsikiliza yeyote mwenye kumkiri. Tuachane na majivuno.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anamponya aliyepooza siku ya sabato. Anapofanya tendo hili, haangalii macho, maneno au usumbufu wa walio karibu. Yeye anajua kwamba jambo jema ni lipi na lazima alifanye. Haogopi macho ya watu. Sisi tuombe kuwa na tabia za namna hii-tuondokane na tabia za kubembeleza urafiki na hivyo tutenda mema. Wapo tunaoogopa kuwaeleza ukweli kwa sababu ni rafiki zetu. Marafiki wa namna hii leo tuwafuate na kuwaeleza ukweli kwamba ni mahali gani wanapokosea. Tusiogope macho yao au tusitishwe na urafiki wao kiasi cha kushindwa kuwaeleza ukweli.

Maoni


Ingia utoe maoni