Jumanne, Januari 18, 2022
Jumanne, Januari 18, 2022.
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa
1Sam. 16:1-13
Zab. 89:19-21, 26-27 (K) 20
Mk. 2:23-28
MAISHA YASIO UNGWA, MAISHA MAPYA
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza linatuletea tafakari ya kupakwa mafuta kwa Daudi kuwa mfalme kwa taifa la Israeli. Daudi anachaguliwa kwa macho ya kimungu, katika kuchagua miongoni mwa wana wa Yese, waliofikiriwa kwamba wanafaa hawakuwa chaguo la Mungu. Mungu amemchagua Daudi, aliye mdogo kati ya wana wa Yese, pia aliyekuwa aliyekuwa mchunga kondoo.
Huyu alionekana kufaa mbele ya macho ya Mungu. Lakini wale walioonekana kufaa mbele ya macho ya Samweli, hawa hawakuwa chaguo la Mungu. Hakika macho ya wanadamu yana makosa mengi. Mwanadamu huangalia umbo, huangalia umaarufu, huangalia urafiki. Lakini Mungu anaangalia mambo kiundani zaidi. Basi tujifunze juu ya udhaifu wa akili ya kibinadamu. Inapokuja kwenye suala la kuchagua, hata mchumba, yafaa tutulie, tusiangalie ya nje sana. Mwombe Mungu utazame ya ndani. Wapo ambao mioyo yao imetawazwa tayari na wanao ruhusu roho wa Bwana wakae ndani yao. Hawa ndio wa kuchagua kama Daudi anavyochaguliwa.
Ujumbe huu uwasaidie na wote wenye kuchagua wachumba. Wengi wetu tunachagua wake kwa kuangalia sura za nje sana, tunachagua wale ambao ni warefu, weupe bila kutambua kilichopo moyoni mwao, hata wanawake huchagua waume wenye pesa au mrefu, mwenye kifua kipana nk, anaweza kuwa na haya yote lakini hajui hata kusali na wala hampendi Mungu ukabaki ukilia maisha yako yote.
Hivyo tujifunze kusali kwanza kabla hata ya kuchagua viongozi wetu. Kiongozi anaweza kuwa mzuri katika kujieleza lakini akawa na utendaji sifuri. Vitu vyema vyatoka kwa Bwana na sio kwa jinsi wanavyoonekana machoni pa wanadamu.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anawajibu Wafarisayo kwamba Mwana wa adamu ndiye Bwana wa Sabato. Pia anasisitiza kwamba Sabato ilichaguliwa ili imsaidie mwanadamu akue kiimani, ili mwanadamu aupate utakatifu.
Kwa kusema hivi, anamaanisha kwamba upendo ndio unaopaswa kuongoza kila kitu, unapaswa kugusa maisha yetu na nyanja zote. Hivyo, tunaposoma somo hili, tujifunze kuzishika sheria zote za kanisa katika upendo. Tusikubali sheria yote ya kanisa iwe kandamizi kwa muumini wake bali sheria hiyo imsaidie aishi kwa amani, upendo, kuwajibika na utulivu zaidi.
Wale wote wanaohusika katika kufundisha na kuhamasisha kuhusu sheria za kanisa wajitahidi wazidishe upendo zaidi ya yote. Unaweza kuwa unasisitiza sheria zaidi na ukakosa upendo watu huchoka haraka na pengine kukosa upendo kwa kanisa. Sheria yetu ni upendo mengine yote hujengwa juu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni