Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Januari 14, 2022

Januari 14 2022.
------------------------

IJUMAA, JUMA LA 1 LA MWAKA

ST. ANTONY ABBOT

Somo la 1: 1 Sam 8:4-7,10-22 Israeli wanataka Mfalme wao, wanakataa utawala wa Mungu.

Wimbo wa katikati: Zab 88: 16-19 Wanafuraha wanao kukiri wewe Ee Bwana kuwa Mfalme, wanaotembea katika mwanga wa uso wako.

Injili : Mk 2:1-12 Yesu anamponja mtu aliyepooza waliye mpitisha juu ya dari.

-------------------------

WAKATI MUNGU AKIWA KIMYA

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Tafakari ya Neno la Bwana katika somo la injili, tunakutana na Bwana Yesu amezungukwa na watu wengi kiasi kwamba ni vigumu kwa wengine hasa wanaokuja nyuma kumfikia. Walio na shida ya mgonjwa aliyepooza wanaamua kufanya uamuzi, tena wa garama kubwa wa kutoboa dari, wanaharibu nyumba ambayo haijulikani ni ya nani-yawezekana hawakujua mmiliki wa nyumba hiyo-lakini wanakuwa tayari kuchukua aumuzi wa namna hii licha ya kwamba ni uamuzi wenye kuhitaji sadaka kubwa. Wanapofanya hivi, Bwana Yesu anaona nia na shida yao na kumponya huyu aliyepooza.
Yawezekana kwamba aliyekuwa mgonjwa alikuwa mtu mashuhuru, au mtu tegemezi katika familia au jamii na ndio maana walikuwa na nia kubwa namna hii. Kwa hakika huu ni uamuzi uliohitaji sadaka kubwa. Yesu anamponya huyu aliyepooza na pia anamwondolea dhambi zake kuonesha kwamba Yesu ni mganga sio tu wa mwili bali na roho; kwani uponyaji ulio mkuu kuliko wote ni ule uponyaji wa Roho. Unaweza kuponywa kimwili lakini kiroho usipoponyeka kwa hakika inakuwa kazi bure. Yesu ndiye mwenye uwezo wa kutenda hili.
Waalimu wa sheria badala ya kuona uzuri ulio katika tendo kubwa la Yesu la kumponya huyu aliyepooza, bali wapo kwenye kutafuta makosa. Ukiishia kuangalia makosa tu hakika utashindwa kutoa uamuzi wa kufaa kuhusu wenzetu. Tutaishia kuongea mabaya juu yao tu. Ndugu zangu, kabla ya kusema baya kuhusu chochote, tuanze pia kwa kuangalia uzuri, ukianzia kutaja lile baya kwanza kwa hakika tunaonekana kuwa watu wa chuki na tutashindwa kutunza nafsi za wenzetu.
Sisi tujitahidi kuungama dhambi zetu kwani kwa kufanya hivi, tunajipatia tiba ya roho yenye kuijenga na miili yetu pia.
Katika somo la kwanza, wana wa Israeli baada ya kuishi katika nchi ya ahadi, imefikia mahali wanaanza kuonesha tamaa ya kutaka kufanana na mataifa mengine. Wanataka kuongozwa na mfalme wa kibinadamu, ili wawe kama mataifa mengine. Walifikiri kwamba mataifa mengine hufaidi zaidi kwa kuwa na wafalme wa kidunia, Samweli anawapa hasara na madhara ya kuwa na wafalme wa dunia lakini wao wanakataa kusikia maonyo yake na kufikiri kwamba bado watapata faida toka kwa wafalme. Lakini Israeli alichovuna toka kwa wafalme wake hakikuwa kitu. Wafalme waovu ndicho chanzo cha wao kuja kupelekwa hata utumwani. Ufalme wa mwanadamu walioutegemea ulileta shida zaidi kuliko furaha.
Sisi tuepukane na kutamani kila yanayotendeka kwa mataifa au familia au jamaa nyingine. Turidhike na hiki chetu tulichopewa. Tamaa nyingi ndio chanzo cha maanguko yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni