Jumatano, Januari 12, 2022
Januari 12, 2022.
------------------------------------------------
JUMATANO JUMA LA 1 LA MWAKA
Somo la 1: 1 Sam 3:1-10, 19-20 Samuel anasikia sauti ya Mungu na kusema “Nena Bwana kwakuwa mtumishi wako anasikia”
Wimbo wa katikati. Zab: 39:2,5,7-10 Nipo hapa Bwana, kuyafanya mapenzi yako
Injili: Mk 1:29-39 Yesu anamponya mtu aliyekuwa na pepo mchafu
------------------------------------------------
UTUME WA YESU
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika neno la Mungu tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na wito wa Samweli-Samweli akiitwa kuwa nabii katika Israeli. Cha kushangaza ni kwamba Samweli aliitwa na Bwana mara mbili lakini yeye hakutambua kwamba ni Bwana; alitambua kwamba ni mwanadamu anamuita-yaani Eli. Na huyu Eli ndiye aliyeweza kumwambia, kumuongoza na kumwambia kwamba ni Mungu anamuita. Katika injili, tunakutana na Yesu akitafutwa na kila mtu, akiitwa na kila mtu-na wanafunzi wake wanamueleza kwamba kila mtu anakutafuta hapa. Lakini yeye baada ya kuwafanyia kazi nyingi, anawaambia kwamba ninapaswa kwenda mahali pengine.
Sauti hizi zinazoniita zinapaswa kuridhishwa na kile nilichowafanyia. Sasa ni wakati wao wa kutumikiana wao kwa wao na kuishi kile nilichowafundisha. Yesu anaitii sauti ya Baba ndani mwake.
Ndugu zangu, tukichunguza masomo yetu ya leo, tunajifunza yafuatayo-cha kwanza, kwa kweli katika maisha yetu, tunamhitaji Eli. Hii ni kwa sababu mara nyingi Mungu amekuwa akituita sisi tukafikiri ni wanadamu na kwa kuwa tulifikiri ni wanadamu wanatuita-huwa hatuzipatii uzito hizo sauti kwani tungejua kwamba ni Mungu anatuita-nakwambia labda tungejibu kwa haraka na kwa umakini lakini kwa sababu tumekosa akina-Eli-tumeishia kufikiri kwamba hizi sauti ni za wanadamu na hivyo kutokuzichukulia kwa makini.
Lakini kuweza kuwa Eli yabidi kujitahidi. Wazazi wengi leo sio wakina Eli. Tukisikia mtoto anatamani utawa labda tunamkataza-tunampelea shule ambayo tena si hata ya kidini ili lengo lake lipotee kabisa. Halafu kama wazazi au sisi mapadre, au walezi kama maadili yetu, au imani yetu ni sio mazuri, kwa kweli hatutaweza kuwa akina Eli. Na ndiyo maana wengi tumewapotosha watoto wetu.
Tumepotosha wito wao na maadili yao na kushindwa hata kuyakubali maisha ya watakatifu. Tumeishi na masuria, bila ndoa, nyumba ndogo yote hayo tumewakwaza watu wakaishia kuikataa sauti ya Mungu nakubaki na maumivu makubwa nakudharau mambo matakatifu.
Katika Injili, Yesu anaonyesha kwamba wakati mwingine sio wa kufuata sauti za ulimwengu. Yesu angefuata sauti za ulimwengu na kuacha kufanya ule wajibu wa kazi yake ya kuuhubiri ufalme, angeishia kumilikiwa na watu wachache tu, wamwambie baki hapa na hivyo kushindwa kuwafikia wengine. Hivyo, Yesu hakufuata sauti ya kila mtu ulimwenguni kwani angeshindwa kutimiza lengo lake.
Hapa Yesu anatueleza kwamba duniani kunahitajika bado akina Eli wa kutufafanulia ipi sauti ya Mungu na ipi sio. Wengi tumepotea au kushindwa kuzichukulia sauti za Mungu kwa makini kwa sababu ya kukosekana kwa akina Eli. Tuombe kuwa akina Eli watakao onesha kwamba hii ni sauti ya Mungu na hivyo ifuate kama Samweli na hii ni sauti ya duniani na hivyo ikatae kama Yesu anavyozikataa sauti za duniani leo zimtakazo asihubiri ujumbe wa ufalme kwa wengine.
Maoni
Ingia utoe maoni