Alhamisi, Januari 13, 2022
Januari 13, 2022.
------------------------------------------------
ALHAMISI, JUMA LA 1 LA MWAKA WA KANISA
Somo la 1: 1 Sam 4:1-11 Wafilisti wanawashinda Waisraeli na kuchukuwa sanduku la Agano la Mungu.
Wimbo wa katikati: Zab 43:10-11,14-15,24-25 Tukomboe Ee Bwana kwasababu ya upendo wako.
Injili: Mk 1:40-45 Yesu anamponya mkoma.
------------------------------------------------
KUMTAFUTA YESU KWA MOYO WOTE!
Wapendwa, karibuni sana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari ya neno la Bwana katika somo la kwanza, wana wa Israeli wanapatwa na mshangao mkubwa kiimani. Wanarudi nyumbani baada ya kushindwa vibaya: wanashangaa na kuuliza sababu za wao wenyewe kushindwa na Wafilisti tena wakiwa mbele ya sanduku la agano.
Wana wa Israeli wanapopigana vita na Wafilisti, wanaamua kulitanguliza sanduku la agano mbele, kwa kufanya hivi, walitegemea makubwa toka kwa sanduku la Agano kwani sanduku la alAgano ni sanduku la Bwana Mungu wa Majeshi, Mungu mwenye mamlaka makubwa, mwenye jeshi kubwa la malaika.
Katika maisha yao, waliwahi kuona ishara nyingi zikitendwa kupitia sanduku hili. Leo wanapolipeleka mbele ya uwanja wa mapambano vitani, wanategemea makubwa, kwamba washinde vita, kwamba Mungu awapiganie hivyo hivyo kama alivyowahi kufanya hapo zamani. Lakini mambo ya ajabu yanatokea. Israeli inapoteza vita na sanduku la agano linatekwa. Hili ni jambo lililowasikitisha sana na kurudi nyumbani wakiwa katika majonzi makubwa.
Kwa nini wana wa Israeli walishindwa kusaidiwa na sanduku la Agano? Ni kwa sababu wao wenyewe walikosa imani, walitegemea sanduku la agano lifanye kazi kama walivyozoea ushirikina. Lakini sanduku la agano halifanyi kazi mbele yao kwa sababu wao walikosa imani mbele ya Mwenyezi Mungu na waliolibeba walikuwa makuhani wenye dhambi.
Sisi ndugu zangu tujue kwamba imani ndiyo muhimu kwa maisha yetu. Tunapovaa rozari, tunapoweka misalaba katika nyumba zetu tutambue kwamba bila imani, hatutatendewa chochote na misalaba hii. Visakrament, misalaba vitumike kiimani na visichukuliwe kama hirizi.
Pia kila tunapovaa visakramenti hivi, lazima tuungame dhambi zetu pia; na kusali. Hapa ndipo tutakapoweza kukua kiimani.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anamponya mkoma mmoja. Mkoma huyu anaonesha imani kwa Yesu, anajua kwamba Yesu anayo mamlaka ya kuweza kumponya na anajua kwamba mamlaka hii anaweza kuitumia kama anavyotaka yeye mwenyewe. Anaweza kuamua kumponya au asimponye. Lakini hata kama hatamponya, Yesu anazidi kubakia na mamlaka yake na uwezo wa kuponya. Ujumbe huu utufae na sisi ndugu zangu.
Kila tunapokuja mbele ya Yesu, tumweleze kwamba mapenzi yako yatendeke. Wapo wengi wetu tunaokuja kusali mbele ya Yesu huku tukiwa na masharti. Na pale tupatwapo na ugumu baada ya maombi na sala, tunaishia kumdharau Mungu na kusema kwamba hana nguvu au hayupo. Sisi tuepuke upofu huu wa kiimani, tutambue kwamba Yesu anazidi kubakia kuwa Yesu hata pale ambapo nimeomba kitu bila kupata. Yesu ni zaidi ya shida na matatizo yangu.
Napaswa kumheshimu kila wakati na kukubali mapenzi yake yatimizwe maishani mwangu. Pia zipo tabia nilizonazo zinazonifanya nishindwe kukaa na jamii yangu nakunifanya nitengwe kama mkoma, tumwombe Yesu atusaidie tuachane na tabia hizi tuweze kurudi tena kwenye jamii nakufurahia.
Maoni
Ingia utoe maoni