Jumatano, Januari 05, 2022
Jumatano , Januari 5, 2022,
Juma Baada ya Epifania
1Yon. 4:11-18
Mk. 6:45-52
KUWA WATU WASIO NA HILA!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, tunapata kutafakari habari za wanafunzi wa Yesu wakiwa katika hofu kubwa, upepo unawasumbua, unawatesa, wanatumia nguvu zao wakipambana nao bila mafanikio.
Baadaye Yesu anajitokeza katikati yao na wanapomuona wanaongezeka tena katika hofu badala ya kupata matumaini. Wanapiga yowe tena wakifikiri kwamba Yesu ni mzima au pepo mchafu amewavamia. Hofu na wasiwasi waliokuwa nao umewafanya washindwe kumtambua Yesu wakati wa matatizo yao na kumfananisha na mzimu. Ndivyo inavyotokea na kwetu kila siku. Wengi wetu tuna hofu na wasiwasi, hivi ni vitu vibaya sana. Vimetufanya tukose iman na kufanya maamuzi ya ajabu.
Wanafunzi walipokuwa katika hofu wamefanya maamuzi ya ajabu. Sisi tuogope kufanya maamuzi hasa wakati tunapokuwa na hofu na wasiwasi mkubwa. Yafaa kwenda mbele ya Mungu kila ujisikiapo hofu kwani maamuzi yoyote utakayofanya katika hofu na wasiwasi ni maamuzi yaliyokosa imani. Unapokuwa katika hofu, habari inayozunguka kichwani yaweza kuwa ni kuhusu pepo wabaya na watu wenye roho mbaya wakitaka kukudhuru. Kila kitakachotokea utakiona kwa macho ya pekee. Ukiona mjusi chumbani utamwita pepo mchafu, muda wote utatembea katika wasiwasi. Hata chumbani utashindwa kulala peke yako. Tujifunze kupambana na hofu zetu.
Katika somo la kwanza, Yohane anasisitiza kwamba kupendana, na anaeleza kwamba katika pendo hakuna hofu, hakuna kumdhania mwenzako vibaya. Somo hili linatuhimize juu ya hatari ya hofu. Tukitaka kuishi na wenzatu katika pendo, tuepuke kumdhania vibaya na hofu za kila siku. Zipo methali zisemazo kikulacho ki nguoni mwako lakini yafaa kwa hakika kuzichunguza methali za namna hii kabla ya kupokea mafundisho yake. Zaweza kutufanya tushindwe kuishi vyema na wenzetu.
Maoni
Ingia utoe maoni