Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Disemba 27, 2021

Desemba 27, 2021.
------------------------------------------------
JUMATATU, OKTAVA YA NOELI

Sikuu ya Yohane, mtume na Mwinjili

Somo la 1: 1Yn 1: 1-4 Yohane, akiwawakilisha Mitume, anatuambia kwamba msingi wa kuhubiri kwao ni kwa kitu kile ambacho wameona na kusikia”Neno la uzima”.

Wimbo wa katikati: Zab 96: 1-2,5-6,11-12 Bwana ni Mfalme, dunia ifurahie, bahari ishangilie. Furahieni enyi wenye haki katika Bwana, mpeni utukufu wa jina lake.

Injili Lk 1: 26-38 Yohane anaonesha hali yake yeye na Petro ya kufika kaburi la Yesu asubuhi siku ya pasaka na kukuta kaburi wazi.

------------------------------------------------

NENO ALIFANYIKA MWILI KWA AJILI YETU!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo ni sherehe ya Mt. Yohane mtume na Mwinjili. Huyu alikuwa mtume aliyekuwa na uhusiano wa karibu kabisa na Yesu na Yesu alidiriki hata kumwachia Mama yake apate kumtunza.
Alipata kuonyeshwa na Yesu mambo makuu maishani mwake kama tukio la kugeuka sura kwa Yesu mlimani Tabor. Yeye alisafiri na Yesu hadi akamuona akikata roho juu ya msalaba. Ukaribu wake na Yesu ulimwezesha kujifunza mengi juu ya Yesu na yote haya aliyaandika kwenye kitabu chake cha nyaraka tatu.
Kati ya mitume ni yeye tu aliyebahatika kuishi muda mrefu zaidi, yeye hakuuawa kifo dini lakini aliteswa sana hadi uzee wake. Kaisari Domisian alimfunga katika kisiwa cha Patmos na hapo basi aliweza kuandika kitabu cha Ufunuo kuwatia moyo wakristo waliokuwa katika mateso makubwa. Ama kweli alifaulu kulijenga kiimani kanisa la mwanzo kwa mafundisho yake na ushuhuda wake wa kiimani.
Kwenye somo la kwanza tunaona akisisitizia jinsi alivyokutana na Yesu, ambaye ni Neno aliye uzima, Mungu aliyechukua ubinadamu, yeye alipata nafasi ya kumuona, akamgusa kwa mikono yake mwenyewe na kula naye chakula. Huyu ndiye Yesu. Maneno haya yalisemwa kuwatia moyo wakristo wachanga ambao walishindwa kuelewa jinsi Kristo ilivyowezekana kwa Mungu kuzaliwa na kuishi kama mwanadamu. Huyu mtume anawaambia kwamba iliwezekana kabisa, na sisi wenyewe tulimuona huyu Neno na tunayo sababu ya kutoa ushuhuda kwa kile tulichokiona.
Hii ndio imani ya Yohane ndugu zangu. Itusaidie na sisi ambao hadi leo bado tunajiuliza kama hawa wakristo wa mwanzo-je, iliwezekanaje? Yohane anakueleza kwamba iliwezekana, yeye mwenyewe aliona kwa macho, akala naye, pia akasikia sauti ya Mungu toka mbinguni ikisema naye. Sisi tuzidishe imani kwa Yesu, yeye ndiye neno wa uzima.
Katika injili, tunaona upendo aliokuwa nao huyu Yohane kwa Yesu, yeye alipopata habari za ufufuko wa Yesu, alikuwa mwanafunzi wa kwanza kwenda kaburini. Ama kweli alimpenda Yesu, alijihusisha sana na Yesu, kila mahali alipenda kwenda naye na ndio maana aliweza kushirikishwa mambo makuu kabisa yamhusuyo Yesu. Sisi tutembee na Yesu, tupende kusoma Biblia, tusali, tujihusishe na habari zake na mambo yake yote. Hakika tutaweza kumtambua zaidi, na atakuja kwetu na kujifunua kwetu.
Yesu anashindwa kujifunua kwetu kwa sababu habari na stori tunazozipiga kila siku ni za vijiweni tu, labda ni matusi tu, labda ni kusengenya tu. Stori za namna hii zinatuzuia kumfahamu Yesu na mwishowe kushindwa kubarikiwa naye. Sisi tutamani kubarikiwa na Yesu kama Yohane na tangu leo tujihusishe naye, kwa kukaa mazingira tuwezayo kuongea naye, na maneno tuwezayo kuongea naye.

Maoni


Ingia utoe maoni