Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Disemba 24, 2021

Ijumaa, Desemba 24, 2021,
Juma la 4 la Majilio

2 Sam 7: 1-5, 8-12, 14, 16;
Zab 88: 2-5, 27, 29;
Lk 1: 67-79

MATAMANIO YAKO YATAKATIFUZWE

Ndugu wapendwa, karibuni kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Neno la Mungu leo katika somo la kwanza, tunamsikia Mungu akimwahidia mfalme Daudi mambo makubwa kwamba moja ya uzao wake atakuwa mfalme milele, na ndiye atakayeleta ahueni kwa Israeli.

Daudi aliweza kuahidiwa hili kutokana na wazo lake jema, wazo la kutaka kumjengea Bwana hekalu, alijitafakari na kuona aibu kwamba alikuwa akilala nyumba nzuri kuliko nyumba ya Mungu na hivyo basi akaamua kusema atamjengea mwenyezi Mungu hekalu.
Mungu aliridhika na nia yake tu na kwa kweli aliishia kubarikiwa namna hii. Yeye alikuwa mfalme wa kwanza kutamani kumjengea Mwenyezi Mungu nyumba na ikapelekea kuahidiwa urithi wa kifalme uliodumu milele.

Hapa tupate somo ndugu zangu. Kuna wakristo baadhi unakuta tunatoka nyumba nzuri lakini wanasali kwenye kigango chenye nyasi. Wanatoka kwenye marumaru wanaenda kusali kwenye makuti-au wanatokea kwenye makochi halafu wanaenda kukaa juu ya mawe au majamvi. Na unakuta baadhi ya wakristo ni waseremala lakini hatujaribu hata kutengeneza kabati au kiti cha kanisani. Na wanaridhika tu, wanakalia viti vichafu. Hii ni kujinyima baraka. Au unakuta wewe unatoka nyumba safi halafu unaenda kanisani kukaa sehemu chafu; unakuta wewe ni meneja wa benki au mhusika usafi wa taasisi fulani lakini pale kanisani kwako ni pachafu kweli. Halafu tunaridhika tu.

Nabii Hagai anasema wengi wamelaaniwa kwa sababu wameitelekeza nyumba ya Bwana. Huyu Daudi alipata kubarikiwa kwa kuijali nyumba ya Bwana. Sisi tusiitelekeze nyumba ya Bwana. Au ukija kudeki kanisani, hudeki vizuri kama kule chumbani kwako, unadeki tuu alimradi umalize.
Katika somo la injili, tunakutana na unabii wa Zakaria. Anakiri kwamba Bwana hakika haachi kutimiza ahadi zake. Ametupatia Mwokozi aliyemzao wa Daudi atakayekuja kutukomboa.

Jana tuliona kwamba nchi lazima ifunguke ili iweze kumpokea huyu Mwokozi, isipofunguka, huyu Mwokozi anakuja tu na kupita. Wengi anakuja na kupita kwa sababu mioyo yetu haijafunguka. Imefungwa na dhambi bado. Tuwe tayari tumpokee Bwana wetu.

Maoni


Ingia utoe maoni