Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Disemba 12, 2021

DOMINIKA YA 3 YA MAJILIO, MWAKA C

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu Jumapili ya leo ambapo ni jumapili ya tatu ya majilio mwaka C wa kanisa. Hii huitwa pia Jumapili ya furaha kwani kipindi cha majilio kimefikia zaidi ya nusu sasa, na Bwana aliye ukombozi wetu yupo karibu kabisa-Bwana hageuki tena katika nia yake, amekwishaamua kuja kutukomboa na nia yake haigeuki tena nyuma.

Masomo yetu yametuandaa kabisa kwenye kutafakari furaha hii. Wimbo wa kwanza unatualika tufurahi katika Bwana. Haya maneno yapo pia kwenye somo la pili. Ni maneno aliyosema Paulo kwa kanisa la Philip. Ni kanisa lililokuwa karimu sana kwa Paulo katika uenezaji wake wa Injili na Paulo alilipenda sana. Leo anaongea nao kirafiki kama watu walio katika imani kubwa wakimsubiria Bwana Yesu arudi kwao kwa haraka kwa mara ya pili na hakika angaliwapatia tuzo kubwa kwani wao walikuwa kanisa aminifu kwa Kristo na lenye tumaini kubwa kwake.

Hivyo hakika Bwana asingaliiacha kabisa bila kuwapatia tuzo. Anawasisitizia wabakie katika matumaini kila wakati kwani hakika Bwana atakuja kwao. Wakipatwa na shida wamweleze Bwana, na wabakie kuwa watu wa shukrani, kusali na kuomba kila wakati. Huu ni ujumbe anaomueleza kila mkristo siku ya leo kwamba lazima tufurahi na kubakia kuwa watu wa matumaini, tayari Bwana alikwishakuja kwetu, na atakamilisha kile alichokianza alipokuja kwa ile mara ya kwanza.

Tubakie watu wa matumaini na wa kupeleka shida zetu zote zinazotusibu maishani mbele ya Bwana. Hii itatupatia matumaini yetu hadi ile siku Bwana atakapokuja kwetu. Huu ndio ujumbe wa muhimu kwa siku hii ya leo ndugu zangu.

Wimbo wa katikati unatoka katika Isaya 12. Huu ni wimbo wa ukombozi na maneno yake yanafanana na ule wimbo aliouimba Musa na Haruni na Miriamu baada ya kuivuka ile bahari ya shamu salama na kuwaacha Wamisri pembeni katika kifo.

Wimbo huu leo unaimbwa ili kutuletea furaha kwamba hakika Mungu kweli ni ukombozi wetu kwa tendo lake la kutaka kumtuma mwanae wa pekee aje kwetu kutukomboa. Tunayo kila sababu ya kufurahi kwani nasi tutakombolewa hivyo hivyo.

Basi ndugu zangu, tupeleke furaha hii kwa wenzetu pia. Kila ulipo tangaza amani leo, usiifiche amani yako au furaha yako ukitaka uifurahie wewe mwenyewe tu, unajidai kununa kuwaonyesha wenzako ati tunateseka kama nyie kumbe ndani umeficha amani yako au pesa zako na unajidai ati hutaki kutoa kicheko chako. Kishirikishe kwa wenzako, acha unafiki wa kujificha.

Somo la kwanza leo linatoka katika kitabu cha nabii Sefania. Linatualika kufurahi pia. Furahi ewe binti Sayuni, piga kelele, kwa sababu kosa la Israeli limefutwa, adhabu yao imeondolewa, na ukombozi umetangazwa kwa upande wao. Israeli aliangushwa na dhambi za uabudu sanamu, na kuchanganya na dhuluma. Sasa nabii anatangaza kusema kwamba kosa hili limeondolewa, afurahi na kupiga kelele. Yeye ataondolewa utumwani.

Ndugu zangu, nasi tunahitaji ukombozi; ukombozi wa kwanza unaanza kwa sisi kusamehewa makosa na Bwana. Dhambi ndio iliyomwangusha mwanadamu. Hivyo tujue kwamba ukombozi unaanza kwa kuondolewa dhambi. Hata kama unataka kumtoa pepo mtu fulani-kwanza aanze kwa kuyakiri makosa yake na kuomba msamaha mbele ya Mungu na hapo basi ndio hatua nyingine ziendelee. Sisi tusiache kuanza kwa kuziungama dhambi zetu. Tukiwa na dhambi hatutaweza kujenga chochote ndugu zangu. Tujitahidi. Hata pepo wenyewe watatutesa ajabu.

Pili ukombozi hupatikana kwa kuwa na amani na mwenzako, kwa kusamehewa makosa na hawa wenzetu. Bila kuwa na amani na wenzako katika jamii huna ukombozi wowote uliokufikia. Utaishi kwa hofu tu. Sisi tuwaombe msamaha wenzetu tukijua kwamba hii ni hatua muhimu kwenye ukombozi wetu.

Tatu ni kwamba ukombozi upo katika kuwafanya wengine wafurahie kwa sababu ya uwepo wako wewe. Ukombozi ni utume, utume wa kuwakomboa wengine. Huwezi kusema kwamba umefikiwa na ukombozi halafu mwenyewe huwezi kumfanya mwingine aokoke, ni lazima tuweze kupeleka furaha hizi kwa wenzetu na ndio tuseme ati tumekombolewa na sisi ndugu zangu. huwezi kuwa mtu wa kuficha vitu vyako, na kuchunachuna halafu useme ati umekwishapokea ukombozi. Wewe hakika bado utakuwa kwenye hali mbaya sana ndugu zangu.

Basi ukombozi sio katika kukaa kimya, kuona kitu kinaharibika halafu hatusemi chochote, tunakaa tu kimya na hatuonyeshi kujishugulisha.

Katika injili Yesu ameorodhesha namna ya kupeleka furaha ya ukombozi kwa wengine. Yohane anapowabatiza askari au watoza ushuru, anawaeleza kwamba ati sio kwamba waiache kazi yao, wanapaswa kuzitakatifuza, waache kuiga, wazitumie kuwapatia wengine huduma.

Ukweli ni kwamba wakristo tunaharibu kwa sababu ya kuiga, tunaingia mahali tunakuta kazi fulani ndani kuna rushwa na halafu mara moja na sisi tunakwenda kujiunga na kupokea rushwa vilevile. Yohane anawaeleza kwamba mnapaswa kuzifanya kazi zenu ziwe mfano, watu wa mataifa wakiwaona na wao wabadilike na mkishakuwa waaminifu wapo watakaowatetea tu na kuwafurahia.

Yesu alipenda ile serikali ya Kirumi, ibadilishwe na maneno kama haya. Wakristo wa mwanzo walifanikiwa kuibadilisha ile serekali ya kipagani ikawa ya Kikristo kutokana na kuishi maneno haya ya Yohane.

Sisi tukumbatie maisha ya huduma, huruma na amani na hakika tutaongoa wengi.
Basi tusiogope kutumia mitandao ya kijamii ati ndani yake kuna uhuni, sisi tuibadilishe iwe ni sehemu ya kushirikishana neno la Mungu kama baadhi wanavyofanya leo na hakika utaona mchango mkubwa upatikanayo kwenye vyombo hivi ndugu zangu. Tatizo ni kama utaingia ndani ya vyombo hivi kwenda kutafuta udaku, na picha mbaya ndio utaanguka. Ingia ndani yake kutafuta neno la Mungu nawe utafanikiwa.

Kila mmoja pia ajue kwamba kwenye kazi au wajibu wake kuna vitu vya kuacha. Watoza ushuru waliambiwa waache kutoza cha ziada. Sisi nasi vipo vingi vya kuacha. Labda manesi acheni kutoa lugha chafu
Lakini zipo na kazi za kuacha kabisa, kama wewe ni mwizi acha, hiyo sio kazi. Takatifuza kazi hiyo. Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni