Jumapili, Novemba 28, 2021
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu dominika ya leo. Leo ni dominika ya 1 ya Majilio. Kipindi hiki kimegawanywa katika makundi mawili. Kwanza ni hadi tarehe 16 December ambapo masomo hutuelekeza juu ya ujio wa pili wa Masiha kwa mara ya pili yakitualika kutubu na kuanzja 16 hadi 24 ambapo tunakumbuka ule ujio wa Kristo kwa mara ya kwanza ulimwenguni. Hivyo kipindi hiki huanzwa kwa utafakari wa ujio wa Kristo kwa mara pili ulimwenguni.
Tafakari yetu inaongozwa na zaburi ya wimbo wetu wa katikati, zaburi ya 25. Hapa tunakutana na maneno Ee bwana nakuinulia nafsi yangu. Hii ni zaburi ya mtu aliyekatika upweke, kakimbiwa na kila mtu, marafiki wake wa zamani hawapo tena. Hivyo anamkimbilia Mwenyezi
Mungu kwa msaada.
Anatambua kwamba kwa njia ya kusali, kujinyenyekeza, na kuungama, ataiokoa nafsi yake, hii zaburi ilikuwa ni kilio cha Daudi baada ya kupinduliwa na mtoto wake aliyeitwa Absalom. Alikimbiwa na marafiki wake wakubwa kama akina Ahitopheli, akabakia kwenye upweke. Hivyo alimlilia Mungu kwa unyenyekevu na kuomba asamehewe na kuonewa huruma.
Zaburi hii inatumika siku ya leo ya jumapili ya kwanza ya majilio kuonyesha kwamba nasi tutaokolewa kwa njia ya unyenyekevu na kumrudia Mungu. Haya ndio yatakayotusaidia kumwona Kristo pale atakapokuja kwa mara ya pili tena.
Katika somo la kwanza, tunakutana na unabii wa Yeremia juu ya wana wa yuda. Kwa kipindi hiki serikali yao ilitawaliwa na wababuloni chini ya Nebuchadnezer. Huyu alikuwa amewapangia cha kufanya-kwamba lazima walipe kodi kwake, wasijidai kwenda kutafuta msaada kwa nchi nyingine ile. Na pale walipokiuka haya, huyu Nebuchadnzer aliwashambulia na kuangamiza mjio wao. Israeli ilikuwa chini ya kiongozi dhaifu, asiye na nguvu. Aliitwa Zedekia. Sasa leo nabii anatabiri kusema kwamba atamchipushia Daudi shina litakalokomboa watu, liongoze watu vizuri, watu wakae vyema, waishi vizuri kwa haki na amani. Ni kama mtu ukae kwenye nyumba yenye uongozi mahiri.
Hili shina ni Yesu ndugu zangu aliyekuwa anasubiriwa. Alitegemewa asiwe kama huyu Zedekia, aliyewaangusha watu, aliyelifanya taifa la Israeli lionekane kuwa dhaifu, lenye kudharauliwa, watu wanakufa kwa njaa na maskini kuonewa. Haya hayatakuwepo pale huyu Masiha atakapokuja.
Ndugu zangu naomba tujifunze kitu toka somo hili.
Sisi tunapaswa kuwa Masiha sehemu tunayoishi hata kama wewe ni Baba wa familia. Ukiambiwa uongoze watu au hata watoto wako, usiwe kama huyu Zedekia. Watu waishi kwa njaa, watoto wako wadharauliwe, wawe machokoraa, washindwe kusoma, waonewe na kila mtu. Hapana, onesha mfano, wafanye waone kwamba yuko Baba, hawanyanyasiki, hawaokoti makombo huko, hawaumwi na kutupwa au kutelekezwa.
Au kama wewe ni kiongozi mahali, usiwaache wale wafanyakazi wako waishi kama ndege, bila 'future', onesha kwamba wewe ni Masiha, wakikueleza shida sio utupilie huko
Lazima Masiha uondoe woga, uwe jasiri; uwe mstari wa kwanza kwenye kutenda. Mfano, kama ni padre, usiogope-labda uletewe mtu mwenye pepo uogope au uogope kuvaa nguo zako au uogope kusali misa tukifikiri ati nitachekwa au kuonwa kuwa mshamba. Sio hivyo, lazima niishi kwa ujasiri. Mtu muoga hawezi kuingia katika ufalme wa mbinguni.
Somo la injili, Yesu anatueleza kwamba kutakuwa na ujio wa mwisho ambapo hukumu itatolewa. Anasisitiza kwamba lazima tuishi kihodari, siku ile isitukute kama wajinga wajinga. Tunaelezwa kwamba siku hiyo isitukute tukiwa tumetawaliwa na vionjo vyetu au anasa zetu. Masiha lazima atawale vionjo vyake. Sio mtu anayekwenda mahali na kukamatiwa hapo kwa sababu hawezi kuiacha.
Nasi kama wakristo, wenye kumsubiri Bwana hatupaswi kutekwa na vitu kama tamaa ya fedha, au sex au pombe kiasi kwamba hadi mwisho utakamatiwa kwenye pombe.
Ni lazima tujifunze kujifanyia control, control ya vyakula, ulafi, vitu vya kutazama. Sio ati ukiona kila filamu utazame, au ukiona kila msichana ulale naye au kila mwanaume, au kila kitu unatamani. Lazima uwe na control, hilo linasisitizwa sana na Yesu.
Zaidi sana ni kutopewa kichwa na visifa vya hapa ulimwenguni, kuna watu akiona anasifiwa kidogo anasahau dhambi zake zote na kufikiri umetangazwa mtakatifu. Hapana, bado kabisa.
Yesu anasema kwamba siku hiyo kutakuwa na ishara, mwezi na nyota zikitikisika. Yaani wale maarufu, wale wanaothibiti au ku-control mambo ya dunia yatatikiswa kabisa, yale wanayoyaona yamuhimu kama jua na nyota. Tujiangalie sisi tunaojiona kuwa na uwezo na nguvu, lazima kuwa wapole zaidi. Sio kila wakati tutabakia kwenye nguvu hizi au uwezo huu. Upo wakati tutaanguka tu.
Maoni
Ingia utoe maoni