Ijumaa, Novemba 19, 2021
Ijumaa, Novemba 19, 2021,
Juma la 33 la Mwaka
1 Mac 4:36-37, 52-59
1 Ny 29: 10-12 (K) 13
Lk: 19:45-48
KUTAKASA HEKALU LA MUNGU
Katika somo la kwanza tunamuona Yuda akipanda pamoja na Askari kwenda mlima Sioni ili kusafisha hekalu. Waandishi wa Kikristo hufananisha hekalu lisilo heshimiwa na roho iliyo jaa dhambi, na hekalu lilosafishwa na moyo uliomrudia Mungu. Hekalu lilikuwa na sehemu nne, kwanza eneo muhimu la kuabudu la makuhani, sehemu ya wanaume, sehemu ya wanawake na sehemu ya watu wa mataifa. Hivyo eneo hili lilibadilishwa na kuwa sehemu ya soko.
Wakati wakuu wa hekalu hawajaingia ndani Yesu aliingia, Yesu aliingia na kuwafukuza wote, kitendo hiki kilikuwa ni ishara kwa watu kwamba Mungu anatuchukulia sala kwa makini sana. Yesu alishikwa na hasira na alisema kwamba “nyumba ya Baba yangu ni nyumba ya sala sio pango la wanyanganyi”. Yesu yupo tayari kung'oa uovu wote kutoka katika hekalu la ulimwengu wetu, na yupo tayari kung'oa uovu wote kutoka katika hekalu la mioyo yetu.
Kila roho ni hekalu ambalo linapaswa kuwekwa tayari kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kutimiza mapenzi yake matakatifu. Kwahiyo Injili hii itatimia kwetu kama tutamruhusu Yesu aingie ndani ya mioyo yetu na kusafisha na kutufanya weupe. Hili linaweza lisiwe jambo rahisi kwani linahitaji unyenyekevu wa kweli na kujikabidhi kwake kweli lakini mwisho wake utakuwa ni kutakaswa na kuwa safi kwa ajili ya Bwana wetu. Wakati Roho Mtakatifu alivyokuja kwetu kwa njia ya utabatizo alisafisha dhambi zote na kutufanya hekalu la Mungu. Kwa msaada wake tunapaswa tuhakikishe hekalu hili halichafuliwi. Kwani tunatambua kuwa kila tunapotenda dhambi tuna muumiza Mungu.
Tafakari leo kwamba Yesu anataka kutuletea utakaso katika njia zetu. Anatamani kulisafisha kanisa pia, kila jamii na jumuiya, familia yako na roho yako mwenyewe. Usikubali utakaso wa Yesu wenye nguvu takatifu ukupite. Sali kwa utakaso wa kila namna na kwa kila ngazi na mwache Yesu atimize utume wake..
Sala:
Bwana, ninasali kwa ajili ya utakaso wa ulimwengu wetu, kanisa letu, familia yetu, na zaidi sana moyo wangu. Ninakualika wewe uje moyoni mwangu uweze kufunua kile kinacho kuhuzunisha wewe sana. Ninakualika uweze kukingoa ndani yangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni